NEWS

Saturday, 2 August 2025

Nyambari Nyangwine: Nichague niunganishe Tarime Vijijini na dunia



Kada wa CCM, Nyambari Nyangwine, akieleza sera zake katika moja ya mikutano ya wajumbe wa kura za maoni za ubunge jimbo la Tarime Vijijini leo Agosti 2, 2025.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

Mgombea wa kura za maoni za ubunge katika Tarime Vijijini kupitia chama tawala - CCM, Nyambari Nyangwine, amezidi kupata umaarufu mkubwa kwa wajumbe, hasa kutokana na sera yake kuu ya kuliunganisha jimbo hilo na dunia.

"Nichague niunganishe Tarime Vijijini na dunia,” amesisitiza Nyambari katika mikutano ya kujinadi kwa wajumbe wa kura za maoni za CCM katika jimbo hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Oktoba 29, 2025.

Wachambuzi wa masuala ya siasa na uongozi wanaitaja sera hiyo ya Nyambari kuwa ni dira ya maendeleo na mustakabali mwema kwa wananchi wa Tarime Vijijini.

Nyambari anayejipambanua kama kada mtiifu wa CCM, mbunifu na mwenye maono makubwa, anatumia sera hiyo kama mwito kwa wananchi wanaotamani kuona mabadiliko ya kweli katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, umeme, mawasiliano, viwanda, kilimo cha kisasa na fursa za ajira kwa vijana.

Amesisitiza kuwa anataka Tarime Vijijini iwe sehemu ya dunia ya kisasa yenye mawasiliano ya haraka, huduma bora na uchumi wa kisasa unaowezesha wananchi kujikwamua kutoka lindi la umaskini.

Kwa kuzingatia sera yake hiyo ya kipekee, Nyambari amejikita katika kutangaza ajenda ya kuunganisha jimbo hilo na ulimwengu kupitia miradi mikubwa ya TEHAMA, ujenzi wa barabara za kisasa, vituo vya afya vya mfano, maboresho ya shule na kubuni mazingira bora ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Kwa wapenda maendeleo, wanachama wa CCM na hasa wajumbe wa kura za maoni, huu ni muda wa kufanya uamuzi wa kihistoria kwa kumchagua kiongozi mwenye maono, uwezo na uthubutu wa kulifikisha jimbo pale linapostahili kuwa - katika dunia ya fursa na ushindani.

Mbali na siasa, Nyambari Nyangwine ni mfanyabiashara, mwandishi na mchapichaji wa vitabu maarufu nchini, ambaye amepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010 hadi 2015 Kwa tiketi ya CCM.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages