
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizindua ghala ma mauzo ya vipuli vya mitambo mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini, jijini Dar es Salaam.
-----------------------------------------
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Tanzania inajipanga kuwa kitovu cha utengenezaji wa bidhaa na huduma za migodini katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vya huduma hizo kwenye migodi ya ndani na nje ya nchi.
Waziri Mavunde aliyasema hayo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam wakati akizindua ghala la mauzo ya vipuri vya mitambo mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini linalomilikiwa kwa ushirikiano wa kampuni za Shan Parts Africa ya India na ITR ya Italia.
“Nawapongeza sana kampuni ya Shan Parts na ITR kwa uamuzi wa kuwekeza nchini Tanzania kwenye vipuri vya mitambo mikubwa na vifaa vya uchimbaji madini.
“Uwepo wa huduma hii hapa nchini utapunguza uingizaji wa vipuri kutoka nje ya nchi kwa wingi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu. Kuwa na huduma kama hii itasaidia sana kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.
“Tumetenga eneo la Buzwagi, Kahama kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani na huduma migodini. Lengo ni kuhakikisha tunaifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa na huduma migodini ndani ya nchi na kwa nchi jirani zinazozunguka nchi ya Tanzania,” alisema Mavunde.
Nao Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Ney na Balozi wa Italia, Giuseppe Coppola, walipongeza ushirikiano wa kibiashara wa nchi tatu - Tanzania, India na Italia, na kuahidi kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na kukuza sekta ya madini ambayo ni muhimu kwenye kuchochea ukuaji wa uchumi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Shan Parts Africa Ltd, Malhar Dave, alisema mazingira mazuri ya uwekezaji chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamewezesha kampuni hiyo kuamua kuwekeza hapa Tanzania, huku akibainisha kuwa mpango wa kampuni ni kuhakikisha inasambaza vipuri vyenye ubora wa hali ya juu kuendana na mazingira ya teknolojia ya dunia ya leo na hivyo kuchochea katika ukuaji wa sekta ya madini.
No comments:
Post a Comment