
Christopher Kangoye (wa pili kushoto waliokaa) ambaye ni mwakilishi wa mgeni rasmi Jackson Kangoye, akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi St. Luka wilayani Tarime wakati wa mahafali ya watoto hao jana.
-----------------------------------------
Mdau wa maendeleo Jackson Christopher Kangoye ameahidi kuipatia Shule Msingi ya St. Luka English Medium iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara vifaa mbalimbali vya michezo ili iwe mfano wa kuigwa.
Jackson ambaye pia ni kada kijana wa chama tawala - CCM ambaye ametia nia ya ubunge katika jimbo la Tarime Mjini mwaka huu, aliwakilishwa na baba yake mzazi, Christopher Kangoye, kama mgeni rasmi katika Mahafali ya Pili ya Darasa la Saba ya shule hiyo yenye mchepuo wa Kiingereza.
"Jackson amenimbia kuwa atashirikiana nanyi kujenga na kufanya shule hii kuwa ya mfano hapa Tarime katika michezo, atashiriki kukuza vipaji vya vijana maana michezo ni ajira.
Aliongeza: "Tunalo jukumu la kuwasaidia, ameniambia kama mtakubali yupo tayari kuwa mlezi wenu katika michezo kuangalia namna gani ya kujenga michezo hapa Tarime, na wazazi tuwaunge mkono walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya," alisema Chiristopher Kangoye.

Mwakilishi wa mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mmoja wa wahitimu wa darasa la saba shuleni hapo jana.
----------------------------------------
Kwa upande wake binafsi, mzazi huyo wa Jackson aliahidi kuipatia shule hiyo msaada wa jezi za mpira kama sehemu ya kumuunga mkono mgeni rasmi, yaani Jackson.
Alitumia nafasi hiyo pia kuihimiza shule hiyo kuzingatia pia elimu ya kujitegemea ili iweze kuwasaidia watoto wanaohitimu na kurudi katika jamii.

Wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi St. Luka English Medium wakifurahia picha ya pamoja wakati wa mahafali yao jana.
-------------------------------------
Awali, Mwalimu Mkuu wa shule ya St. Luka, Sista Theresia Odira, alisema mahafali hayo ni ya wanafunzi 34 (wasichana 17 na wavulana 17) wanaotarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu darasa la saba Septemba 2025.
Pia, katika risala yake kwa mgeni rasmi, Sista Theresia aliweka wazi kuwa shule hiyo inaongozwa na Shirika la Masta wa Moyo Safi wa Maria Africa, chini ya Jimbo Katoliki la Musoma.
“Malengo ya shule hii ni kutoa elimu na malezi bora, kufundisha maadili mema na uzalendo kwa taifa letu, lakini pia kuwapunguzia wazazi na walezi adha ya kupeleka watoto wao nje ya nchi kufuata elimu inayotolewa kwa lugha ya Kiingereza,” alisema Sista huyo.
Mwakilishi wa mgeni rasmi katika picha ya pamoja na Bodi ya Shule ya Msingi St. Luka English Medium wakati wa Mahafali ya Pili ya Darasa la Saba ya shule hiyo jana Agosti 14, 2025. (Picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment