
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, akizindua upanuzi mradi wa chanzo cha maji unaotekelezwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara leo Agosti 21. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na katikati ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko.
-----------------------------------------
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, leo Agosti 21 amezindua mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji kilichopo Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa vijiji vingine vipatavyo saba vinavyozunguka mgodi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.665 za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) zilizotolewa na mgodi huo - unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Akizungumza baada ya kukagua na kuzindua mradi huo, Ussi ameipongeza Barrick kwa jinsi inavyojali huduma bora za kijamii na maendeleo ya wananchi.
Aidha, Ussi ameipongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi ya maji.
“Hatukuona changamoto yoyote ya miradi ya maji tangu tuingie katika mkoa huu - na tumeridhika kwa asilimia 100 juu ya utekelezaji wa miradi hii,” amesema Ussi.

Awali, Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mohamed Mtopa, amemweleza kiongozi huyo wa mbio za Mwenge kwamba mwanzoni chanzo hicho cha maji kilisanifiwa kuhudumia wakazi 27,742 wa vijiji - Nyangoto, Matongo, Mjini Kati na Nyabichune.
Lakini kutokana na ongezeko la mahitaji ya maji katika vijiji saba vinavyozunguka mgodi wa North Mara, chanzo hicho kilisanifiwa upya kwa lengo la kuhudumia wakazi 125,566 katika vijiji vya Kewanja, Genkuru, Nyamwaga, Nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mtopa, mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 80, utaongeza uzalishaji kutoka lita 2,314,000 hadi 10,213,000 na hivyo kufikia lengo la serikali la mwaka 2020-2025 la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio vijijini.
Mradi huo unatarajiwa kuwaondolea wakazi wa vijiji husika adha waliyokuwa nayo ya kutumia muda mrefu kutafuta maji, ambapo sasa watapata muda wa kujielekeza kwenye shughuli za uzalishani mali na kukuza uchumi wao.
Mapema, pamoja na miradi mingine, Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Ussi, amezindua zahanati ya kijiji cha Mangucha katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - ambayo pia imejengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara.



Kikundi cha ngoma ya asili kinachofahamika kwa jina la Nyakitari kikitoa burudani wakati wa uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.


No comments:
Post a Comment