NEWS

Monday, 18 August 2025

Panga la CCM la mchujo kwa wagombea Ubunge, Viti Maalum kuanza kazi Alhamis

 Katibu wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na MAfunzo, CPA Amos Gabriel Makala

Na Mwandishi Wetu


Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itakutana Dodoma Alhamis wikii hii kuchuja wagombea Ubunge wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge wa Viti Maalum, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Wabunge wa Baraza la Wawakilishi wa Viti Maalum.


Taarifa iliyotolewa jana jijini Dodoma na Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya chama hicho ilisema kuwa kikao cha Kamati Kuu kitafuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Jumamosi kuthibitisha majina ya wagombea wa nafasi hizo kama yalivyopitishwa na Kamati Kuu.


Vikao vyote viwili vya chama hicho tawala vitakuwa chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, kama inavyooneshwa kwenye ratiba ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.


Mpaka sasa, CCM tayari ilishafanya uteuzi wa awali wa wagombea wa majimbo na viti maalum kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano -- Tanzania Bara na Visiwani.


Sasa ngoma nzito inatarajiwa kwenye mchujo wa mwisho wa wagombea Ubunge na Viti Maalum kutokana na ushindani mkali , hasa baada ya CCM kuongeza idadi ya wagombea kwa majimbo baada ya kuifanyia marekebisho Katiba yake.


Katika baadhi ya majimbo kuna wagombea kuanzia watano hadi saba, jambo linaloashiria kwamba kutakuwepo mchuano wa kukata na shoka kwa wagombea kupenya tanuru la mchujo.


Huenda mwaka huu pia ukashuhudia mchuano mkali kwa nafasi ya wagombea Urais baada ya vyama vya upinzani zaidi ya 10 kutaja wagombea wake.


Kinyang'anyiro cha kuwania kukamata dola kitadhihirika zaidi wakati wa kampeni za miezi miwili zinazotazamiwa kuanza rasmi nchi nzima Agosti 28.


Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi Julai 1, 1992, CCM imeendelea kukamata dola kwa kuibuka mshindi katika chaguzi zote kuanzia 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020.


Mtandao mpana ulioenea nchi nzima unaipa nafasi kubwa CCM kuibuka mshindi ikilinganishwa na vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa vikipambana kuangusha mbuyu bila mafanikio.


Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages