NEWS

Sunday, 21 September 2025

DC Haule akagua maendeleo ya utekelezaji Mradi wa Maji wa Miji 28



Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Tarime-Rorya juzi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha.

Na Mwandishi Wetu
Rorya
-----------

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Rorya, Dkt. Khalifan Haule, amekagua Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Tarime-Rorya na kuutaja kama moja ya miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa na serikali katika mkoa wa Mara.

"Huu ni mradi mkubwa sana kwa mkoa wetu wa Mara, kwanza napenda kumshukuru Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha zinazowezesha ujenzi wa mradi huu kuendelea,” Dkt. Haule alisema mara baada ya kukagua mradi huo Septemba 19, 2025.

Mradi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 134, utawezesha maelfu ya wananchi wa wilaya za Rorya na Tarime kuanza kufuharia huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria.

Mfano, Dkt. Haule alisema karibia asilimia 90 ya wananchi wa Rorya katika kata 21 watanufaika na mradi kwa kupata huduma ya maji safi na salama.

Katika ziara hiyo, Dkt. Haule alifuatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Rorya na watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) na Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Kiongozi huyo alikagua ujenzi wa tenki litakalokuwa na ukubwa wa kuhifadhi maji lita milioni sita lililopo eneo la Kowak na kituo cha kuchuja maji kinachojengwa katika kata ya Nyamagaro.


Ukaguzi wa mradi huo ukiendelea

"Kamati imepata nafasi ya kutembelea kwenye ujenzi wa tenki la maji (Kowak) na baadaye tumekuja kwenye chanzo na hapa shughuli zinaendelea vizuri,” alisema Dkt. Haule.

Alihimiza mkandarasi wa mradi huo kuoneza kazi ili kukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi wa Rorya wanaze kufurahia huduma ya maji kutoka Ziwa Victoria.

Dkt. Haule alibainisha kuwa Kamati ya Usalama ya Wilaya yake imejipanga kuhakikisha usalama wa kutosha kwa vifaa vya ujenzi wa mradi huo.


Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha, akizungumzia maendeleo ya mradi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages