NEWS

Saturday, 20 September 2025

FZS yaendesha warsha ya ushauri wa muundo wa kushughulikia malalamiko ya jamii kwa miradi yake



Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco Lubela (kulia waliokaa) na DED Serengeti, Dkt. Mauled Suleiman Madeni (kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Shirika la FZS mjini Mugumu hivi karibuni.

Na Mwandishi Wetu
Serengeti
--------------

Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) limeendesha warsha ya siku mbili ya ushauri wa kitaalamu wa muundo wa majaribio ya utaratibu wa kushughulikia malalamiko ya jamii kwa miradi yake katika wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.

Warsha hiyo ilifanyika Septemab 10-11, 2025 mjini Mugumu, Serengeti, washiriki wakiwa ni pamoja na wenyeviti na maofisa watendaji wa vijiji vitano vya majaribio – Robanda, Bokore, Bonchugu, Merenga na Makundusi vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi wilayani humo.

Washiriki wengine walikuwa wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori IKONA (IKONA WMA), maofisa kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Kupitia warsha hiyo, FZS ililenga kupata maoni ya wadau kuhusu muundo wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ili kuhakikisha unazingatia mazingira halisi ya jamii, matarajio ya wananchi kwa misingi ya uwazi, haki na usawa.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza imani ya wananchi kwa FZS, kuboresha mawasiliano na ushirikiano kati ya jamii na shirika hilo, na hivyo kuimarisha utekelezaji wa miradi yake.

Akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Angelina Marco Lubela, aliipongeza FZS kwa kuandaa warsha hiyo yenye mwelekeo wa kuboresha zaidi uhusiano na jamii.

“Kwa hili la kusikiliza malalamiko ya wananchi mnamuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na litasaidia kupunguza migogoro baina ya jamii na wahifadhi,” alisema DC Lubela ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Serengeti, Dkt. Maulid Suleiman Madeni.


DED Serengeti, Dkt. Madeni, akisisitiza jambo katika warsha hiyo.

Akiwasilisha mada katika warsha hiyo, Afisa Ulinzi wa Jamii kutoka FZS, Digna Irafay, alisema mfumo wa kuupokea na kushughulikia malalamiko ya jamii ni daraja kati ya jamii na taasisi za uhifadhi na wafadhili.

“Mfumo huu unasaidia kuondoa kero mapema… Kukosekana kwa mfumo wa malalamiko wananchi hukosa imani na kupunguza dhamani ya miradi,” alisema Digna.


Afisa Ulinzi wa Jamii kutoka FZS, Digna Irafay, akiwasilisha mada katika warsha hiyo.

Kwa upande wake, mtaalamu wa mifumo ya kushughulikia malalamiko ya jamii kutoka INCAS Consulting, Miriam Byekwaso, alisema mfumo huo ni takwa la kimataifa ambapo wafadhili wanataka fedha wanazotoa zilete maendeleo, siyo migogoro katika jamii.

“Lengo la mfumo wa kusikiliza malalamiko ni kuisaidia jamii iondokane na hali duni,” alisema Miriam na kusisitiza kuwa mafanikio ya miradi ya wafadhili yanategemea kwa kiwango kikubwa uhusiano mzuri na jamii.

Naye Meneja Mradi wa FZS - Serengeti, Masegeri Rurai, alisema shirika hilo linaamini katika nguvu ya ushirikiano na mawasiliano kwa uwazi, hivyo mfumo huo utakuwa chombo muhimu cha kujenga uaminifu na uwajibikaji kati yao na jamii zinazozunguka maeneo ya uhifadhi.


Meneja Mradi wa FZS - Serengeti, Masegeri Rurai, akizungumza katika warsha hiyo.

Kwa upande wao, washiriki wa warsha hiyo walionesha ari na utayari wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa majaribio ya mfumo huo, huku wakiahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa FZS katika utekelezaji wa hatua zinazofuata.

Walitumia fursa hiyo muhimu kutoa michango ya mawazo na mapendekezo yao kuhusu namna bora ya muundo wa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya jamii kwa wakati, haki na njia inayoheshimu haki za binadamu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bonchugu, Simion Mahando, alisema mfumo huo utasaidia kuwaondolea wananchi changamoto ya kuwasilisha maoni yao kuhusu miradi inayotekelezwa na FZS katika maeneo yao.

“Tumepokea kwa furaha warsha hii, imetujengea uwezo na tunaamini mfumo huo wa kushughulikia malalamiko utaisaidia pia FZS kujua na kutekeleza miradi inayohitajika kwa jamii,” alisema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Robanda, Yohana Mzalendo.

Warsha hiyo ni sehemu ya mikakati ya FZS ya kuhakikisha kuwa miradi inayoitekelezwa inakuwa jumuishi, endelevu na yenye kuwianisha mahitaji ya watu na mazingira.

Awali, Meneja wa Uendeshaji kutoka FZS, Edmund Tobico, alisema shirika hilo la uhifadhi linafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za serikali, zikiwemo TANAPA, TAWA na halmashauri za wilaya.


Meneja wa Uendeshaji wa FZS, Edmund Tobico, akizungumza kwenye warsha hiyo.

FZS ni Shirka la Uhifadhi la Kimataifa lenye makao makuu nchini Ujerumani ambalo limekuwa likisaidia Serikali ya Tanzania katika kuimarisha masuala ya uhifadhi, huku uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ukiwa moja ya vipaumbele vya shirika hilo kwa takriban miaka 60 sasa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages