NEWS

Saturday, 20 September 2025

Kamishna wa Uhifadhi atia neno kikao cha wafanyakazi TANAPA Investment



Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Nassoro Kuji.

Na Mwandishi Wetu
-----------

Wafanyakazi wa kampuni tanzu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) inayojulikana kama TANAPA Investment Limited (TIL), wametakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi zao kufuatana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ili huduma zao za ukandarasi wa ndani na nje ziwe bora zaidi.

Kampuni ya TIL ilianzishwa 2019 ili kutoa msukumo kwa miradi ya TANAPA pamoja na kuwa kitega uchumi kwa taasisi hiyo ya serikali.

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Nassoro Kuji, amewataka wafanyakazi hao kuwa na mshikamano, ushirikiano, upendo na nidhamu katika kutimiza majukumu yao kwa taifa.

Kuji aliyasema hayo Alhamisi iliyopita alipokutana na wafanyakazi hao kwenye kikao cha kawaida cha kazi, ambapo aliwamwagia sifa kwa utendaji wenye ufanisi - pongezi ambazo pia zilitolewa na Bodi ya Wadhamini ya TANAPA.

“Bodi imenituma niwaeleze kuwa ina matarajio makubwa sana kwenu na hivyo msiwaangushe,” Kamishna Kuji alisema.

TIL ni kampuni iliyokarabati barabara ya Hifadhi ya Taifa Arusha na kipande cha barabara ya Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kuzifanya barabara hizo kupitika kwa urahisi.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa TIL, Mhandisi Richard Matolo, aliahidi kwamba kampuni hiyo itaongeza kasi katika utendaji wake ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Mhandisi Matolo alisema kampuni hiyo ni nyenzo madhubuti ya kuhakikisha kwamba miundombinu ya hifadhi inatunzwa katika hifadhi za taifa ili kuchochea uchumi unaotokana na shughuli za utalii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages