NEWS

Thursday, 25 September 2025

Peter Mutharika: Profesa aliyeshinda mashtaka ya ulaghai na kurejea madarakani


Miaka mitano baada ya kuondolewa mamlakani kupitia uamuzi wa mahakama, Peter Mutharika anajiandaa tena kurejea madarakani kama Rais wa Malawi.

Mutharika, ambaye aameshikilia nyadhifa za juu kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, ameshinda uchaguzi mkuu uliofanyika wiki iliyopita, baada ya kumpiku hasimu wake wa muda mrefu, Rais Lazarus Chakwera.

Wakiti wa kampeni Mutharika aliwaambia wapiga kura kwamba maisha bila shaka yatakuwa mazuri chini ya uongozi wake - Malawi imekumbwa na mdororo mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa tangu Chakwera aingie madarakani.

Lakini utawala uliopita wa Mutharika mwenye umri wa miaka 85 pia haukusazwa, kwani ulikumbwa na madai ya rushwa ambayo yalimfanya kufurushwa uongozini baada ya kuhudumu kwa muhul ammoja.

Hii ni mara yake ya nne amewania nafasi hiyo, lakini awali Mutharika hakukusudia kuingia kwenye siasa.

Alizaliwa mwaka wa 1940 katika eneo la Thyolo linalosifika kwa ukuzaji wa majani chai. Alilelewa na walimu wawili ambao walimfanya kupenda elimu.

"Nilikulia katika familia ambayo wazazi wangu walikuwa waelimishaji, na mimi mwenyewe nilitumia maisha yangu yote katika elimu ya juu, katika vyuo vikuu saba katika mabara matatu," Mutharika alisema mnamo 2017, wakati wa hotuba katika Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza.

Alisemea katika Sya Dedza, taasisi iliyoko katikati mwa Malawi inayojulikana kwa kulea wanasiasa mashuhuri, na alisomea sheria katika miaka ya 1960 katika Chuo Kikuu cha Yale nchini Marekani.

Mutharika aliendelea kuwa profesa, akijenga utaalamu katika haki za kimataifa. Alitumia miongo kadhaa mbali na Malawi akifundisha katika vyuo vikuu vya Marekani, Tanzania, Uganda na Ethiopia.

Hatimaye Mutharika alijihusisha na siasa mwaka 2004, wakati kaka yake mkubwa, Bingu, alipokuwa rais wa Malawi.

Mutharika alirejea nyumbani kuhudumu kama mshauri wa rais mpya na mwaka 2009, alichaguliwa kuwa mbunge wa chama tawala cha Democratic Progressive Party (DPP).

Alihudumu katika baraza la mawaziri la kaka yake kama waziri wa sheria, waziri wa elimu na kisha waziri wa mambo ya nje.
Mutharika alitoka kwa wanafunzi na kumbi za mihadhara na kuwa kuungana na viongozi kwenye ziara za serikali
Mutharika alipanda ngazi ya mamlaka kwa amani, lakini mvutano uliibuka mwaka wa 2010, baada ya madai kuibuka kwamba Bingu alipanga kumtaja kaka yake kama mgombea urais wa DPP katika uchaguzi wa 2014.

"Kila wiki, machifu kutoka kila pembe ya nchini walionekana kwenye televisheni ya taifa wakiimba nyimbo za kumsifu Peter Mutharika... hatua hiyo ilizua ghadhabu, baadhi ya watu wakisema huu ni upendeleo wa wazi," mwanahabari wa Malawi Francis Chuma aliandika katika gazeti la The Guardian.

Lakini mipango ya urithi ilisambaratika ghafla Aprili 2012.

Akiwa na umri wa miaka 78, rais alipatwa na mshtuko wa moyo, na kufariki. Mutharika alitoa heshima za dhati kwa marehemu kiongozi huyo kwenye mazishi yake, akimtaja kama "kaka yangu, rafiki yangu na pia shujaa wangu".

Baada ya wadhifa wa Urais kuachwa wazi, mzozo wa madaraka ulianza. Katiba ya Malawi ilisema iwapo mkuu wa nchi atafariki akiwa madarakani, makamu wa rais atachukua nafasi hiyo, lakini Bingu alitofautiana na makamu wake, Joyce Banda, kuhusu mipango tata ya kumpatia wadhifa huo kaka yake.

Chama cha DPP kilikuwa kimemfukuza Banda, ambaye baadaye alianzisha chama kipya, People's Party (PP), lakini akakataa kuachia nafasi ya makamu wa rais.

Rais alipofariki, wafuasi wake walijaribu kumweka Mutharika kama kiongozi kinyume na katiba, lakini hatimaye Banda alishinda na kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Malawi.

Mutharika alishtakiwa kwa kosa la uhaini baada ya kutuhumiwa kuwa sehemu ya njama ya kuficha kifo cha kaka yake ili kumpa muda wa kufanya njama ya kumzuia Banda kushikilia wadhifa wa urais.

Alitupilia mbali mashtaka hayo kuwa ya kipuuzi na ya kisiasa - na yaliondolewa baada ya kuchaguliwa kuwa rais mwaka wa 2014, na kuwashinda Banda na Chakwera kwa zaidi ya asilimia 36 ya kura.

Wafuasi wa Mutharika wanasema kuwa nafasi yake ya kwanza madarakani iliiinua Malawi, ikiashiria mabilioni ya dola za mikopo ya China aliyopata ili kurekebisha miundombinu ya nchi hiyo.

Mfumuko wa bei pia ulipungua sana wakati wa muhula wa kwanza wa Mutharika. Alipomrithi Banda, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 24% - hadi anaondoka, ulikuwa umepungua kwa hadi tarakimu moja.

Lakini utawala wa Mutharika pia ulikumbwa na visa vya kukatika kwa umeme, uhaba wa chakula na kashfa za ufisadi ambazo kwa muda mrefu zimekumba siasa za Malawi.


Mamo mwaka wa 2018, shirika la kupambana na rushwa la Malawi lilimshutumu Mutharika kwa kupokea rushwa kutoka kwa kandarasi ya kwacha ya 2.8bn ($1.6m; £1.2m) ya kusambaza chakula kwa polisi.

Wamalawi waliingia barabarani kuandamana lakini baadaye aliondolewa makosa.

Amekuwa akijitetea mara kwa mara kama mtetezi wa vita dhidi ya ufisadi na ubadhirifu, akiambia BBC mwaka wa 2015 kwamba alikuwa "rais pekee barani Afrika anayesafiri kibiashara".

Ingawa Mutharika alistahimili madai ya ufisadi, aliishia kupoteza urais katika moja ya nyakati za kushangaza katika historia ya kisiasa ya Malawi.

Mutharika aliwania muhula wa pili mwaka 2019 na baada ya kura kuhesabiwa, alitangazwa mshindi.

Hata hivyo, Mahakama ya Kikatiba baadaye ilibatilisha uchaguzi huo, ikisema kumekuwa na uingiliaji mkubwa.

Majaji waliamuru kurudiwa kwa uchaguzi wa 2020 na, cha kushangaza, Chakwera alishinda kwa 59% ya kura.

Mutharika alitaja marudio hayo "kutokuwa halali", Mahakama ya Katiba ilipata sifa ya kimataifa kwa kulinda demokrasia na kukataa kushawishiwa na mamlaka ya rais.
Peter Mutharika akiapishw akwa muhula wa pili madarakani 2019, lakini aliondolewa madarakani kupitia uammuzi wa mahakama ambao haukutarajiwa.
Alitangaza kuwa hatagombea tena nafasi hiyo, lakini aliwashangaza wengi alipojiunga tena na kinyang'anyiro cha urais mwaka huu, akisema wafuasi wake wanamtaka ainusuru nchi dhidi ya Chakwera.

Tangu Mutharika aondoke madarakani, mfumuko wa bei umepanda hadi 30%. Kimbunga Freddy, ukame mbaya, kupungua kwa hifadhi ya kigeni na miongoni mwa mambo mengine yamewafanya Wamalawi kukabiliwa na umaskini.

Wakati wa hotuba za kampeni mwaka huu, Mutharika aliwauliza wafuasi wake kwa lugha ya kichichewa: "Munandisowa eti? Mwakhaula eti? (Unanikosa sio? Umeteseka, sivyo?)".

Lakini Mutharika alionekana mara chache hadharani wakati wa kampeni, tofauti na Chakwera ambaye alifanya mikutano mingi nchini Malawi.

Kutokana na hali hiyo, uvumi kuhusu afya ya Mutharika ulienea huku maswali yakiibuka ikiwa ana uwezo wa kuiongoza Malawi tena akiwa na umri wa miaka 85.

Bila kujali, wapiga kura wameweka imani yao kwake. Alishinda hata katika maeneo yaliyoonekana kuwa ngome za Chakwera, kama vile mji mkuu, Lilongwe, na Nkhotakota.

Ingawa safari yake ya kisiasa imekabiliwa na matukio mengi, maisha ya kibinafsi ya Mutharika ni tulivu. Shirika la habari la AFP linamtaja kama "aliyetengwa" huku Mail & Guardian ya Afrika Kusini ikiandika kwamba "marafiki wanasema yeye ni mtu wa kusoma, anayependa starehe zaidi na vitabu kuliko mikutano ya kisiasa".

Mutharika ana watoto watatu kutoka kwa mke wake wa kwanza Christophine, ambaye alifariki mwaka 1990. Mnamo Juni 2014, alimuoa mbunge wa zamani wa DPP, Gertrude Maseko.

Wanandoa hao wanatazamiwa kurejea katika makao ya rais, lakini safari hii ya Mutharika itakuwa na uzito zaidi.

Wamalawi wengi wameteseka, kama Mutharika alivyobainisha katika hotuba zake za kampeni. Kwa hiyo mavumbi ya kurejea kwake yasiyotarajiwa yatakapotulia, taifa litakuwa likitazama, kwa hamu kuona kama atatimiza ahadi yake ya kuwarudisha kwenye nyakati bora zaidi.
Chanzo:BBC

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages