NEWS

Saturday, 20 September 2025

Malalamiko ya wananchi yapungua Mgodi wa Barrick North Mara



Lori likiwa kazini katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara

Na Mwandishi Maalumu
Tarime
-----------

Idadi ya malalamiko ya wananchi inayofikishwa katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara imeshuka kwa kiwango kikubwa, mgodi huo umesema.

Takwimu zinaonesha malalamiko yaliyofikishwa katika mgodi huo imeshuka kutoka 57 mwaka 2024 hadi 11 Septemba 2025.

Mgodi wa North Mara una kitengo maalum cha kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusiana na shughuli za uchimbaji wa madini ambacho kipo katika ofisi zake za Mahusiano.

Inaelezwa kuwa malalamiko yote yaliyopokewa mwaka jana yalishughulikiwa kwa mafanikio makubwa.

Kushuka kwa idani ya malalamiko ya wananchi kunatokana na jitihada ambazo Barricki imekuwa ikifanya kutatua changamoto ambazo ilizikuta mara baada ya kukabidhiwa kuendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

“Malalmiko yameshuka sana, mfano kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi sasa [Septemba 2025] tumepokea malalamiko 11 na yamepungua sana,” alisema Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Francis Uhadi hivi karibuni.

Francis alisema hayo katika sehemu ya taarifa yake kwa Timu ya wataalamu wa Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) iliyotembelea mgodi huo.

Alisema mgodi huo umefanya kazi kubwa kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwepo na hivyo kufanikiwa kuondoa mambo yaliokuwa yanasababisha sehemu kubwa ya malalamiko.


Watalaamu kutoka TEITI wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa waandimizi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara walipofanya ziara katika mgodi huo hivi karibuni.

Mei 2025, mgodi huo uliendesha kliniki ya kusikiliza malalamiko na maoni mablimbali kutoka kwa wakazi wa vijiji 11 vinavyouzunguka.

“Tuliendesha kliniki na kusikiliza malalamiko kwa kila kijiji,” Francis aliwaeleza wataalamu hao kutoka TEITI.

Katika miaka ya karibuni, mgodi wa North Mara umekuwa chachu ya maendeleo kwa vijiji vinavyouzunguka kwa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za kijamii na kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya wajibu wake kwa jamii (Corporate Social Responsibility - CSR).

Mgodi huo pia umeendelea kutoa fursa za kibiashara na ajira kwa mamia ya Watanzania wakiwemo wanaotoka vijiji jirani, ikiwa ni sehemu ya mpango wake kabambe wa kutekeleza sera ya ‘local content’ kwa vitendo.

Lengo la ziara ya wataalaamu hao kutoka TEITI ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa Sheria ya Madini upande wa CSR na Ushirikishwaji wa Watanzania yaani ‘Local Content’.

Ujumbe huo wa TEITI ulitembelea pia miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha za CSR na kueleza kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na kampuni ya Barrick katika kuchangia maendeleo ya Watanzania.

TEITI ni taasisi ya serikali inayohamasisha uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ili kuhakikisha mapato yanayotokana na rasilimali hizo yanakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya Watanzania na taifa kwa ujumla.

Mgodi wa Barrick North Mara uliopo katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara unatajwa pia kuwa kuendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kutoka sekta ya madini nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages