NEWS

Thursday, 18 September 2025

Mara: Tume ya Haki za Binadamu yalikumbusha Jeshi la Polisi kuepuka kuwa chanzo cha kuvuruga amani kwenye uchaguzi




Na Ada Ouko
Musoma
------------

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini imelikumbusha Jeshi la Polisi kuepuka kuwa chanzo cha kuvuruga amani wakati wa kampeni zinazoendelea na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Wito huo ulitolewa na Kamishna wa Tume hiyo, Dkt. Thomas Masanja, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na Jeshi la Polisi mjini Musoma,Mkoa wa Mara jana Septemba 18, 2025.

Dkt. Masanja alisema jeshi hilo linaweza kuwa chanzo cha kuvuruga amani na kuchafua taswira ya nchi ikiwa halitazingatia taratibu na sheria.

Kamishna Dkt. Thomas Masanja

“Tunakutana na Jeshi la Polisi kwa lengo kuwakumbusha wajibu wao kipindi hiki cha uchaguzi, na sana sana tunasisitiza kwenye madhara yanayoweza kutokea kama hawatazingatia taratibu na sharia za utekelezaji wa majukumu yao.

“Kwamba wanaweza kuwa chanzo cha kuvuruga amani kama hawatazingatia taratibu zao, lakini wanaweza kuchafua taswira ya nchi kama hawatazingatia taratibu zao na sheria.

“Lakini vilevile, tutakutana na waandishi wa habari kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara kuwakumbusha wajibu wao na kuwasisitiza kutumia kalamu zao vizuri, lakini wawe ni wahamasishaji wakubwa wa wananchi kwenda kupiga kura, kuwajulisha haki yao na wazingatie sharia na taratibu.

“Kubwa zaidi wawambie wananchi kwamba wana haki ya kupiga kura na kushiriki kwenye kampeni zinazoendelea ili mwisho wa siku waweze kuchagua viongozi bora watakaojali maslahi yao,” alisema Dkt. Masanja.

Awali, alisema Tume hiyo inafuatilia utekelezaji wa haki za binadamu na utawala bora kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, tangu wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hadi wakati huu wa kampeni, kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

“Katika kufuatilia huko tunakutana na wadau mbalimbali - wananchi kwa kuhusisha vyombo vya habari, hasa redio jamii,” Dkt. Thomas.

Aidha, alisema Tume hiyo imepanga kukutana waandishi wa habari leo Septemba 19, 2025 mjini Musoma kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), ili kuwakumbusha wajibu wao na kuwasisitiza kutumia kalamu zao vizuri.


Mrakibu wa Polisi Mwandamizi, Paul Ngonyani.

Kwa upande wake Mrakibu wa Polisi Mwandamizi, Paul Ngonyani, ambaye ni Msaidi wa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mara, alisema mafunzo ya Tume hiyo yana tija kwa jeshi hilo.

“Yamelikumbusha mambo mengi, ikiwemo utendaji wa kazi zetu za kila siku, yatatusaidia katika kutekeleza majukumu yetu mbalimbali kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu,” alisema Ngonjani.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages