
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Partick Chandi (kulia), akimnadi kwa wananchi mgombea ubunge katika jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.
Na Mwandishi Wetu
Musoma
-------------
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, amefanya ziara maalum katika jimbo la Musoma Vijijini, akihamasisha wananchi kuwachagua wagombea wa chama hicho katika nafasi za urais, ubunge na udiwani.
Chandi amewahimiza wakazi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kukipatia CCM kura za ushindi ili kiendelee kushika madaraka ya nchi - kwa kuzingatia historia yake ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kisekta.

Katika ziara hiyo, kiongozi huyo amefanya pia mikutano ya CCM ya ndani kwenye kata mbili, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwachagua wagombea wa chama hicho tawala, akisema ilani na ahadi zake zinaeleweka na kutekelezeka.

“Mwenyekiti wetu amefanya mikutano ya ndani katika kata za Bugoji na Tegeruka wakati wa kuomba kura za chama chetu,” kilisema chanzo cha habari kutoka ofisi ya CCM mkoani Mara, Septemba 25, 2025.

Mbali na kuongeza hamasa ya ushindi kwa wagombea wa CCM, ziara za Chandi kipindi hiki zinalenga pia kuimarisha chama hicho katika mkoa wa Mara kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Oktoba 29, 2025.

Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazidi kupamba moto nchini kote, huku vyama vya siasa vikipigana vikumbo kuwashawishi wapiga kura kwa sera na ahadi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment