
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda wa siku 90 Leseni ya Huduma za Maudhui Mtandaoni kwa Kampuni ya Vapper Tech Limited maarufu kwa jina la JamiiForums sambamba na kuzuia upatikanaji wa jukwaa la Jamii Forums kuanzia Septemba 6, 2025.
Taarifa iliyotolewa jana Septemba 6, 2025 jijini Dar es Salaam na kutiwa saini na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Kuwe Bakari, imesema Mamlaka hiyo imechukua hatua hiyo kufuatia Jamii Forums kupitia jukwaa lake na akaunti zake za mitandao ya kijamii kuchapisha maudhui ya kupotosha umma, kukashfu na kudhalilisha Serikali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za Mwaka 2000 na Marekebisho yake ya mwaka 2022 na 2026.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa pamoja na kukiuka Kanuni, maudhui hayo yanakinzana na utamaduni, mila na desturi za Kitanzania, jambo linaloathiri umoja, amani na mshikamano wa kitaifa na kuharibu taswira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sura 306, TCRA imepewa mamlaka ya kusitisha kwa muda wa siku 90 Leseni ya Huduma za Maudhui Mtandaoni itakapobaini yanapotosha umma wa Tanzania na kinyume cha maadili ya taifa.
No comments:
Post a Comment