
Jackson Kangoye
Na Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetengua uteuzi na kumwondoa kwenye orodha ya wagombea wa Ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jackson Kangoye ambaye alikuwa mgombea kwa tiketi ya chama cha ACT - Wazalendo katika Jimbo la Tarime Mjini.
Kuondolewa kwa mgombea huyo kunafuatiwa Tume kukubali rufaa ya pingamizi iliyowekwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, Esther Matiko, kuhusu ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi katika kuteuliwa kwa Kangoye.
Tume ilitoa uamuzi wake baada ya kufanyika kwa kikao chake kuanzia Septemba 1 hadi 5 kupitia rufaa 51 zilizofikishwa mbele yake na baadhi ya wagombea kuhusu kukiukwa kwa taratibu za uteuzi na wasimamizi wa uchaguzi.
Pingamizi dhidi ya Kangoye kwa nafasi ya ubunge ni moja ya rufaa nne zilizokubaliwa na INEC wakati nyingine zilitupiliwa mbali.
Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepangwa kufanyika Oktoba 29, 2025 wakati kipindi cha sasa cha miezi miwili kinatumika kwa kampeni za kunadi sera na wagombea kwa kila chama kinachoshiriki kwenye uchaguzi huo.
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Julai 1, 1992, huu utakuwa Uchaguzi Mkuu wa saba chini ya mfumo huo.
No comments:
Post a Comment