
Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia mkutano wa kampeni mjini Mugumu, Serengeti leo Oktoba 10, 2025.
Na Mwandishi Wetu
Serengeti
---------------
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi kuwa mpango wa ujenzi wa uwanja wa ndege Mugumu, wilayani Serengeti utatekelezwa endapo atachaguliwa kubaki madarakani.
Dkt Samia amesema mji wa Mugumu ni wa kimkakati kwa kuwa upo jirani na Hifadhi ya Taifa Serengeti na kusisitiza kwamba ujenzi wa uwanja huo utafanyika ili kukuza utalii na kutengeneza fursa za ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Amesema ujenzi wa uwanja huo utawezesha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti kutua moja kwa moja katika mji wa Mugumu na hivyo kuufanya mji huo kuwa kitovu cha utalii.
Dkt. Samia amesisitiza ahadi hiyo leo Oktoba 10, 2025 wakati akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni mjini humo.

“Hapa Mugumu tunakwenda kujenga kiwanja cha ndege na ipo kwenye ilani… tutajenga uwanja huo ili kuwezesha watalii kutua hapa Mugumu,” amesisitiza Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa ujenzi wa mradi huo utawezesha hifadhi bora Afrika – Hifadhi ya Taifa Serengeti kuzidi kuvutia watalii wengi wa ndani na nje ya Tanzania.
Aidha, hatua hiyo amesema itavuta wawekezaji na itakuwa fursa ya kiuchumi kwa vijana.
Sambamba na hilo, mgombea huyo amesema serikali yake itaendelea kutangaza vivutio vya utalii nchini ili kuongeza idadi ya watalii hadi milioni nane kufikia mwaka 2030.
Dkt. Samia alikuwa akijibu maombi ya mgombea ubunge katika jimbo la Serengeti, Mary Daniel Joseph (CCM), aliyekumbushia mpango wa ujenzi wa uwanja huo, miongoni mwa miradi mingine ya kijamii na kiuchumi.

Mgombea ubunge jimbo la Serengeti kupitia CCM, Mary Daniel Joseph, akizungumza kwenye mkutano huo
Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo pia kumuombea kura mgombea ubunge, Mary Daniel Joseph na wagombea udiwani wote wa CCM katika jimbo la Serengeti.

Kwa mkutano huo wa Mugumu wilayani Serengeti, Dkt. Samia amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara, ambapo mapema leo amehutubia mkutano wa kampeni wilayani Butiama.
No comments:
Post a Comment