
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Stephen Wasira, wakiwa kwenye mkutano mkubwa wa kampeni mjini Bunda, mkoani Mara jana Alhamisi.
Na Mwandishi Wetu
Mara
-----------
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuuletea mkoa wa Mara mageuzi makubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwa atabaki madarakani.
Akihutubia mikutano wa kampeni kwa nyakati tofauti katika miji ya Bunda na Musoma jana, Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliahidi kuboresha zaidi huduma za kijamii na kiuchumi.
Huku akieleza kufurahishwa na wakazi wa Mara kwa namna walivyojitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza, mgombea huyo aliahidi kujenga vituo vya zana kilimo, skimu za umwagiliaji na kuendeleza ruzuku za mbolea na pembejeo.
Kuhusu uvuvi, Dkt. wa urais aliahidi kuongeza ujenzi wa mabwawa na vizimba kwa ajili ya ufugaji wa samaki ili kuwezesha vijana wengi kupata ajira na kuinua uchumi wao.
Aliongeza kuwa uboreshaji wa sekta za kilimo na uvuvi vitakwenda sambamba na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao yanatokana na shughuli hizo ili kuyaongezea thamani na kuleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wa miundombinu ya usafirishaji, Dkt. Samia alisema serikali yake itaweka msukumo kwenye ujenzi na ufufuaji wa bandari na viwanja vya ndege kwa ajili ya kupokea meli na ndege kubwa za kibiashara.
Pia serikali yake itaweka nguvu katika ujenzi wa stendi na masoko ya kisasa ili kupanua fursa za kibiashara na kiuchumi kwa wananchi.
Aidha, aliahidi kuendeleza ujenzi wa barabara za lami mkoani Mara kama ambavyo imeainishwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2025-2030.
Viivile, alisema serikali yake itahakikisha maeneo yote yanafikiwa na huduma bora za maji, afya, maji, elimu na umeme. “Chagueni CCM ili tuyafanyie kazi hayo yote,” aliwaomba wana-Mara.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa, alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Hospitali ya Ruraa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kwanga na Chuo Kikuu cha Mwalimu JK. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia – Butiama.
Hata hivyo, Chandi aliomba kuongezewa msukumo wa ujenzi wa mtandao wa barabara za lami ili kuwahisishia wananchi usafiri mkoani humo.
Katika mikutano hiyo ya kampeni, Dkt. Samia aliambatana na Mkamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Asha-Rose Migiro, miongoni mwa viongozi wengine.
Leo Ijumaa, mgombea huyo anaendelea na ziara ya kampeni katika wilaya za Butiama na Serengeti kuelekea Uchaguzi Mkuui unapangwa kufanyika nchini Oktoba 29, 2025.
No comments:
Post a Comment