NEWS

Wednesday, 15 October 2025

Kenya yaondokewa na mwanasiasa machachari Raila Odinga



Raila Amolo Odinga enzi za uhai

Na Mwandishi Wetu

Kiongozi mashuhuri wa siasa za upinzani nchini Kenya, Raila Amolo Odinga, 80, amefariki dunia nchini India leo asubuhi Jumatano Oktoba 15, 2025 kwa ugonjwa wa moyo.

Kiongozi huyo alikumbwa na mauti hospitali katika mji wa Kochi, kusini mwa India alikokuwa anaendelea na matibabu, kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya habari ya Reuters na CNN.

Siasa za upinzani zilimweka Odinga katika ramani ya dunia baada ya kugombea nafasi ya urais mara tano bila mafanikio.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa 2007 ambapo kulikuwepo mchuano mkali kati ya Mwai Kibaki na Raila Odinga, matokeo yake yalisababisha vurugu na umwagaji damu wa wenyewe kwa wenyewe kabla ya kuzimwa na juhudi za jumuiya za kimataifa.

Juhudi za Raila Odinga kama mwanaharakati wa demokrasia zilizaa matunda nchini Kenya kutokana na mageuzi ya kuanzishwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1991 na kuandikwa kwa Katiba Mpya mwaka 2010.

Raila Odinga alikuwa ni mtoto wa pili wa Makamu wa Rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga (1911-1994), ambaye mwaka 1966 alijitoa katika chama tawala cha Kenya African National Union (KANU) na kuunda chama chake cha siasa cha Kenya People’s Union (KPU) akiachana na uongozi wa Rais Jomo Kenyatta.

Kama wasemavyo Waswahili, mtoto wa simba ni simba, ndivyo alivyokuwa Raila kwa sababu hakurudi nyuma katika siasa za upinzani na amefariki dunia akiwa kiongozi mkuu wa upizani nchini Kenya.

Kwa Afrika Mashariki, jina la Raila Odinga siyo geni katika mapambano ya kudai haki na uhuru na ametangulia mbele za haki watu wengi wakimjua ni “mpambanaji” kama alivyokuwa baba yake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages