NEWS

Monday, 13 October 2025

Serengeti: Mwekezaji wa Grumeti Reserves alivyowezesha upatikanaji eneo litakalojengwa uwanja wa ndege Mugumu



Sehemu ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege Mugumu wilayani Serengeti

Na Mwandishi Maalumu

Thamani ya nia njema iliyooneshwa na mwekezaji wa kampuni ya Grumeti Reserves - ya kusaidia kwa vitendo mpango wa ujenzi wa uwanja wa ndege Serengeti katika mji wa Mugumu, imeonekana baada ya Mkuu wa nchi kuuhakikishia umma kwamba tayari mradi huo umeidhinishwa kwa utekelezaji.

Takriban miaka iliyopita, kampuni hiyo iliunga mkono serikali juu ya mpango huo - kwa kutoa shilingi bilioni 1.1 kuwezesha upatikanaji wa eneo ambapo uwanja huo utajengwa.

Fedha hizo zilitumika kulipa fidia kwa wananchi na uhamishaji wa Shule ya Msingi Burunga ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.

Habari njema zaidi ni kwamba, baada ya kusuasua kwa takriban miaka 20, hatimaye mpango wa ujenzi wa uwanja huo umepewa kipaumbele kwa kuingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025-2030.

Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgombea wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, amewahakikishia wananchi kuwa akirejeshwa madarakani, serikali yake itatekeleza ujenzi wa uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu.

Dkt. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, alisisitiza ahadi hiyo Oktoba 10, 2025 wakati akihutubia mkutano mkubwa wa kampeni katika mji huo.


Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akihutubia mkutano wa kampeni mjini Mugumu, Serengeti wiki iliyopita.

Mbali na kukuza utalii, alisema ujenzi wa kiwanja hicho utavutia uwekezaji zaidi katika wilaya hiyo ambayo imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti na mapori ya akiba ya Ikorongo- Grumeti.

Aliongeza kuwa ujenzi wa uwanja huo utawezesha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani kutua moja kwa moja katika mji wa Mugumu na hivyo kuufanya kuwa kitovu cha utalii.

“Hapa Mugumu tutakuja kujenga kiwanja cha ndege, na kipo kwenye ilani. Tutakijenga ili kuwezesha watalii kutua hapa Mugumu,“ alisistiza Dkt. Samia.

Chandi anavyopigania
ujenzi wa uwanja huo

Huwezi kuzungumzia mpango wa ujenzi wa uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu bila kumtaja Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.

Chandi ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuweka msukumo wa ujenzi wa uwanja huo, alitumia nafasi ya mkutano huo wa kampeni kumshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha fedha za kuanza utekelezaji wa mradi huo.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.

Upembuzi yakinifu waendelea, Dkt. Nyansaho 
Mwenyekiti Kamati ya Ujenzi wa uwanja huo
Tayari Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetiliana saini na Kampuni ya Saba Engineering mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti katika mji wa Mugumu.

Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba huo jijini Dar es salaam Februari 27, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mambokaleo, alisema serikali ilitenga shilingi bilioni 1.3 katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja huo.

Alisema serikali inadhamiria kujenga uwanja huo ili kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti pamoja na kurahisisha usafiri wa wananchi na mizigo kuingia mkoani Mara.

Aidha, Oktoba 7, 2025, timu ya wataalamu kutoka TAA, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Wahadhiri wa Uchumi - Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) walikutana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kujadili na kupata uelewa wa pamoja kuhusu ujenzi wa uwanja huo.

Baadaye timu hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Uwanja huo, Dkt. Rhimo Nyansaho na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Dkt. Maulid Suleimani Madeni, ilitembelea na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi huo katika kata ya Uwanja wa Ndege, nje kidogo ya mji wa Mugumu.


Dkt. Rhimo Nyansaho (katikati) akiongoza timu ya wataalamu kukagua eneo litakalojengwa uwanja huo.

Juhudi hizo za serikali chini ya chama tawala - CCM, zinazidisha matumaini ya kuona ndoto ya ujenzi wa uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu ikitimia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Inaelezwa kuwa ujenzi wa uwanja huo umebuniwa kuwa wa kisasa, ukiwa na hudumu zote muhimu zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kutengeneza fursa za kiuchumi, zikiwemo ajira kwa vijana, huduma za malazi, chakula na usafirishaji - zitakazokuwa na mchango mkubwa katika kuinua kipato cha wananchi.

Hakika, mchango wakampuni ya Grumeti Reserves katika kusaidia upatikanaji wa eneo lililohitajika kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo umekuwa wa thamani kwani umeonesha jinsi sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya taifa.

Grumeti Reserves ni kampuni ya utalii wa kiikolojia - ambayo pia inatajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kusaidia uhifadhi na maendeleo ya jamii katika mfumo ikolojia wa Serengeti pamoja na kutengeneza ajira kwa mamia ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages