
Mgombea Ubunge Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Joseph na Mgombea Udiwani Kata ya Busawe, Ayub Mwita Makuruma, wakiomba kura za CCM wakati wa uzinduzi wa kampeni katani humo Ijumaa iliyopita.
Na Mwandishi Wetu
Serengeti
---------------
Serengeti
---------------
Mgombea ubunge katika jimbo la Serengeti kupitia CCM, Mary Daniel Joseph, Ijumaa iliyopita alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni za kada mwenzake, Ayub Mwita Makuruma, anayetetea kiti cha udiwani kata ya Busawe.
Mary aliwaomba wananchi kukiamini CCM na kuwapigia kura za kutosha wagombea wake wa nafasi za urais, ubunge na udiwani.
Alimtaja mgombea udiwani katika kata Busawe, Makuruma, kama kiongozi mchapa kazi mahiri.
"Naombeni kura za imani na kishindo kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan [mgombea urais kupitia CCM], msipompa kura za kishindo mtaninyima jeuri ya kumfuata na kumwambia ‘Mama hawa watu walikupa imani, ni zamu na wewe kwenda kuwalipa’.
“Mambo ambayo nitayafanya ni ushirikiano na ufuatiliaji maana tayari mnalo jembe la kazi [Makuruma], lazima tuchochee maendeleo Busawe,” alisema Mary.

Kwa upande wake Makuruma alitaja miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi cha uongozi wake na kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
"Tulikuwa na upungufu wa madarasa, shule za Sekondari, lambo la maji, barabara, jengo la mama na mtoto, lakini Serikali ya CCM kupitia kwa Mama [Raid Dkt. Samia] imefanya mambo mengi sana, tuungeni mkono tunakwenda kukamilisha kila kitu kilichobakia.
Aliendelea: "Tunahitaji mafiga matatu ili tuweze kufanya kazi vizuri, niwaombe tarehe 29, Oktoba tujitokeze kwa wingi sana, asiwepo hata mmoja atakayebaki nyumbani, tujitokeze kwa wingi kupiga kura kwa wakati na kurudi majumbani.
"Niseme kwa ujasiri, mkinipa hili jembe - binti wenu [mgombea ubunge], basi mnidai maendeleo, tunakwenda na Mary Daniel kwa nafasi ya ubunge na Dkt. Samia kwa nafasi ya urais," alisema Makuruma.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Japan Mrobanda, alimtaja Makuruma kama kiongozi msikivu na mwenye msimamo mzuri - anayeshirikiana na kila mtu. “Hii ni lulu na neema ya wana-Busawe, 29 Oktoba nendeni mkapige kura za kukiamini CCM, mchagueni Makuruma aendelee kuwa diwani wa kata ya Busawe,” alisema.
No comments:
Post a Comment