
Dkt. Jane Goodall na sokwe
Na Mwandishi Maalumu
Wakati mwingine binadamu akiwa hai na kufanya mambo makubwa huwa hatambuliki KIRAHISI mpaka pale atakapotoweka (kufa) ndipo sifa zake nyingi hujitokeza na kuvuma dunia nzima kumwelezea kwamba naye alikuwepo.
Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Dkt. Jane Goodall, mtaalamu wa primate na kinara wa uhifadhi wa mazingira ambaye alianzisha Kituo cha Utafiti wa Sokwe cha Gombe kilichopo mkoani Kigoma, Tanzania.
Dkt. Goodall alifariki dunia Jumatano Oktoba 1, 2025 huko Los Angeles, Marekani akiwa na umri wa miaka 91.
Huyu ni mwanasayansi maarufu aliyepambanua na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia tangu kwenye ujana wake alipoanzisha utafiti wa sokwe na kupigania kuwanusuru wanyamapori hao katika mazingira wanamoishi.
Ingawa ametangulia mbele za haki, mama huyo sasa amejizolea umaarufu kwa kuandikwa kwa mawanda mapana na magazeti na mashirika ya habari maarufu duniani kama vile New York Times, Reuters na Xinhua, kwa kutaja machache.
Gazeti la New York Times, ambalo ni maarfu duniani tangu karne ya 19 lililopochukuliwa kwa umiliki na uendeshaji na mwandishi gwiji na mchapishaji, Adolph Ochs, limeeleza kuwa watu wengi wanamfahamu Dkt. Jane Goodall kama mhifadhi mwenye nywele nyeupe kichwani ambaye alikuwa akitoa hotuba kwenye Umoja wa Mataifa kupigania hifadhi ya sokwe.

Hata hivyo, kwa wanasayansi, Dkt. Jane Goodall ni mwanataaluma aliyewafuatilia sokwe kwa karibu kwa majuma kadhaa - ambaye sasa amekuwa kielelezo sahihi duniani kwa mambo aliyoyatenda kuhusu uhifadhi wa wanyama hao na utunzaji wa mazingira.
“Daima kutakuwepo na Jane Goodall mmoja tu,” ameeleza Michael Tomasello, mtaalamu wa asili ya lugha katika Chuo Kikuu cha Duke, kama alivyokaririwa na gazeti la New york Times.
Nalo shirika la habari la China la Xinhua limeeleza kwamba Dkt. Jane Goodal aliwasili magharibi mwa Tanzania mwaka 1960 bila ya kuwa na ujuzi wowote lakini kazi yake ya utafiti katika Hifadhi ya Taifa Gombe iliboresha uelewa wa kisayansi kuhusu sokwe na kuchochea harakati duniani za uhifadhi wa wanyama hao na mazingira yao.
Kwa Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa uhai wake alikuwa mtu aliyemshawishi na kumuunga mkono Dkt. Jane Goodall katika utafiti wake wa kuwahifadhi na kuwatunza sokwe katika mazingira yao.
Hii ilikuwa kazi aliyoanzisha mwanamama huyo wakati Mwalimu Nyerere akiwa kwenye harakati za kuleta uhuru nchini Tanganyika (sasa Tanzania).
Dkt. Goodall alishuhudia kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika na kuishi kwa kipindi chote cha kujinyumbua kwa taifa hili kubwa katika Afrika Mashariki – kupitia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, kurejea kwa uchumi wa kiliberali na hatimaye kurejea kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992.
No comments:
Post a Comment