
Somalia inatazamiwa kuanzisha lugha ya Kiswahili katika mtaala wa shule za kitaifa, Rais Hassan Sheikh Mohamud alitangaza jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika Mashariki (EACCON) mjini Mogadishu.
Katika mkutano huo unaohudhuriwa na mamia ya wajumbe, Rais huyo wa Somalia alitoa wito wa kuendelezwa kwa lugha ya Kiswahili.
"Vyuo vikuu vya nchi, hasa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Somalia, vinapaswa kuzingatia zaidi kukuza lugha ya Kiswahili, ambayo ni lugha ya Afrika Mashariki," alisema.
Kwa mujibu wa Rais Mahamud, hatua hiyo ni muhimu kwani hivi karibuni Somalia imekuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. "Kukubali Kiswahili ni muhimu kwa ushirikiano wetu katika kanda," alisema.
Waziri wa Elimu, Farah Sheikh Abdulkadir, pia alisema serikali inashirikiana na taasisi za kikanda kuandaa mfumo wa kukitambulisha Kiswahili nchi nzima.
"Tunajitahidi kuimarisha usomaji na utumiaji wa lugha ya Kiswahili nchini Somalia. Tunataka kuona Kiswahili kinakuwa lugha ya mawasiliano, biashara na kujifunza, hata kuchukua nafasi ya Kiingereza wakati wa mkutano wetu ujao," aliongeza.
Somalia ilijiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2024, na kuwa nchi mshirika wa nane wa umoja huo pamoja na Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Maelfu ya Wasomali wanazungumza Kiswahili, lugha ambayo wamekuwa wakijifunza sana katika miongo ya hivi karibuni.
BBC
No comments:
Post a Comment