NEWS

Wednesday, 8 October 2025

Dodoma: Wataalamu wapendekeza mpango kazi kudhibiti utoroshaji madini




Na Mwandishi Wetu
Dodoma
--------------

Wadau wa sekta ya madini Tanzania wamependekeza kuandaliwa kwa mpango kazi mahsusi ili kudhibiti tatizo linalojitokeza kwa kasi la utoroshaji madini.

Hilo ni moja ya mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na kikao cha pamoja cha wataalamu kutoka taasisi za serikali kilichojadili mikakati ya kukomesha utoroshaji wa madini nchini.

Kikao hicho kilifanyika jijini Dodoma jana Oktoba 7, 2025 chini ya uenyekiti wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo.

Mbibo alisema utoroshaji wa madini ni tishio kwa uchumi na usalama wa taifa, hivyo lazima kuwepo ushirikiano wa hali ya juu kukomesha vitendo vinavyochangia hali hiyo.

Aliongeza kuwa utoroshaji wa madini umekuwa ukiliingizia taifa hasara kutokana na kupotea kwa mapato yake kwa njia haramu.

“Madinji ni miongoni mwa rasilimali muhimu zinazotegemewa kuchochea maendeleo ya taifa letu. Hatuwezi kuendelea kupoteza mapato kwa sababu ya mianya ya utoroshaji. Ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika vita hii,” alisema Mbibo.

Aidha, alipendekeza kuwepo kwa mfumo thabiti na shirikishi wa udhibiti wa madini kuanzia migodini, vituo vya ukaguzi, viwanja vya ndege, bandari na mipaka yote.

“Tunapaswa kuwekeza katika vifaa vya kisasa vya kuchunguza na kubaini madini – hasa madini ya vito kwa haraka na kwa uhakika. Vifaa hivi vitasaidia kuzuia mbinu zinazotumiwa na watoroshaji,”alisema.

Eneo lililopendekezwa katika kukabili utoroshaji wa madini ni kuwepo kwa mafunzo endelevu kwa wataalamu wanaofanya kazi maeneo ya ukaguzi ili kuwajengea uwezo wa kutambua aina mbalimbali za madini, mbinu za usafirishaji haramu na matumizi ya teknlojia ya kisasa katika kukomesha mbinu chafu za watu wanaohusika na biashara haramu ya madini.

Kikao hicho kilichofanyika mji wa serikali wa Mtumba, kilihudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Madini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Tume ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages