
Tembo wakihamishwa kutoka Kyerwa na Karagwe kwenda Hifadhi ya Taifa Brigi-Chato.
Na Jacob Kasiri
Kyerwa
--------------
Operesheni ya kuhamisha tembo takriban 500 kutoka maeneo ya wananchi na mwekezaji wilayani Kyerwa na Karagwe kwenda Hifadhi ya Taifa Burigi-Chato inaendelea kufanikiwa.
Uhamishaji wa wanyamapori hao ambao unatekelezwa kitaalamu bila kusababisha bughudha kwa wananchi na mali zao, unaendeshwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Tayari makundi makubwa mawili ya tembo zaidi ya 100 waliotembea umbali wa kilomita 150 kutoka Kyerwa wameshaingia ndani Hifadhi ya Burigi-Chato na kuonesha dalili zote za kutokurudi walipotoka. Hatua hiyo imekuja baada ya wataalamu wa ikolojia kutoka TANAPA kuyafuatilia makundi hayo kwa ukaribu.
Makundi ya tembo yanahamishwa kila siku kwa kuswagwa kwa kutumia helikopta mbili za JWTZ na magari.
Juzi Oktoba 03, 2025, tembo 105 waliokuwa katika makundi mawili waliswagwa kutoka Kyerwa yalipo mashamba ya mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kagera (Kagera Sugar) hadi eneo la Golini mpakani mwa wilaya ya Kyerwa na Karagwe kwenda Hifadhi ya Burigi-Chato.
Ikumbukwe kuwa Septemba 30, 2025, wakati Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Massana Mwishawa, alipozuru na kushiriki doria ya kuswaga tembo hao, aliridhishwa na maendeleo ya operesheni hiyo.
“…endeleeni kuyafuatilia makundi ambayo mmeyafikisha hifadhini ili yasirudi tena na kwenda kusababisha karaha kwa wananchi na mali zao - japo kwa umbali yaliotembea na misukosuko yaliyoipata ni vigumu kurudi,” alisema Naibu Kamishna Mwishawa.
Naye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda-Kyera, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi (ACC), Fredrick Mofulu, ambaye ndiye msimamizi na mratibu wa operesheni hiyo alisema watahakikisha tembo wote waliosalia wanahamishwa ili kuwaondolea wananchi kero ya kuharibiwa mazao na kuhatarishiwa maisha yao.
Operesheni hiyo pia iliwahusisha Makamishna Waandamizi wa Uhifadhi, Charles Ngende, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe na Catherine Mbena, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TANAPA.
Aidha, operesheni hiyo ilishirikisha taasisi nyingine za uhifadhi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zikiwemo za Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment