Mgeni rasmi, Moses Makindi Jacob (aliyevaa shati jeupe katikati), akikabidhi msaada wa kompyuta kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Getena wakati wa Mahafali ya Kwanza ya Darasa la Saba shuleni hapo Oktoba 2, 2025.
Na Godfrey Marwa
Tarime
------------
Mdau wa maendeleo, Moses Makindi Jacob, ameipatia Shule ya Msingi Getena iliyopo kata ya Nyanungu wilayani Tarime msaada wa kompyuta moja na Seti ya Msaada wa kwanza (First Aid Kit).
Moses ambaye ni mzaliwa wa kata hiyo, pia ameahidi kuipatia shule hiyo msaada wa ‘photocopy machine’, madaftari na kalamu kwa wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani.
Alitoa msaada wa vifaa na ahadi hizo kwenye Mahafali ya Kwanza ya Darasa la Saba shuleni hapo Oktoba 2, 2025, ambapo alialikwa kuwa mgeni rasmi.

Wahitimu wa darasa la saba wakifurahia jambo katika mahafali yao
Mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mhitimu
Septemba 2025, wanafunzi 68 (wasichana 49 na wavulana 19) walifanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi katika shule hiyo mpya yenye madarasa ya kisasa - kuanzia awali mpaka la saba.
Akijibu risala ya shule hiyo ambayo ilioonesha kuimarika kitaaluma kutokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wanafunzi na jamii, Moses alisema wakazi wa kijiji cha Nyamombara wana kila sababu ya kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha za ujenzi wa shule hiyo ya kisasa ambayo sasa inafanya kijiji hicho kuwa na shule mbili za msingi.

Mgeni rasmi akizungumza katika mahafali hayo
"Ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi ukiwepo mtaendelea kufanya vizuri sana, hii ni shule nzuri sana iliyojengwa chini ya uongozi Mama - Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumpongeze kwa kutukumbuka wana-Getena, ni jambo la kujivunia,” alisema Moses.
Aliendelea: "Wanafunzi ambao mpo hapa mimi ni mwenzenu, tumetoka kwenye haya mazingira - tuendelee kujituma, hapo mlipo mwisho wa siku mtakuwa viongozi wakubwa katika nchi hii. Elimu ndio ufunguo wa maisha matokeo yakitoka nitachangia kaunta book tano na kalamu tano kwa kila mmoja wenu.
"Wazazi somesheni watoto ndio wanaoleta weupe (mwanga) nyumbani, wapeni fursa wasome, wanapoenda shule wambieni pia dunia ya sasa ni ya utandawazi, kuna mambo mengi, changanya akili yako na ya kuambiwa.”

Wazazi wakifuatilia tukio katika mahafali hayo

Mgeni rasmi akikabidhi cheti kwa mhitimu
Kuhusu changamoto nyingine, Moses alisema: "Nimeleta kompyuta na First Aid Kit, wakileta umeme - photocopy machine nawaletea kwa kushirikiana na wadau, hizo ndizo shukrani zetu kwenu kama wana-Nyanungu, shirikisheni vijana wenu na wadau kunapokuwa na changamoto katika shule zetu.”
"Kuhusu ukosefu wa umeme, hili nimelichukua na kwa kuanza nalo Mwenyekiti wa Kamati ya Shule na Mwalimu Mkuu tukitoka hapa waje niwapeleke kwa Meneja wa TANESCO, shule nzuri kama hii haiwezekani kukosa umeme wakati nguzo ziko karibu, na ikumbukwe shule hii imejengwa chini ya mradi wa Boost, hivyo ni ya kisasa zaidi,” alisema Moses.

“Hili la madawati tutalifikisha kwa uongozi wa wilaya kwa maana ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na hili la changamoto ya maji tayari serikali yetu pendwa imeshaleta mradi katika kata yetu ya Nyanungu, hivyo kila kijiji kipambane kipate maji pamoja na vitongoji vyake zikiwemo taasisi zilizopo ndani ya kijiji kama hii shule.
"Hii ni shule ya mfano katika kata ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri tukifanya mitihani ya kata ndiyo shule inayoongoza,tukifanya ya wilaya ni miongoni mwa shule zinazoongoza kumi bora niwapongeze walimu wazazi na kamati kwa ushirikiano uliopo,” alisema Moses.
Kuhusu ufinyu wa eneo la shule, mgeni rasmi alisema hilo liko chini ya uongozi wa serikali ya kijiji kupitia vikao na mikutano halali ya wananchi kuangalia ni namna gani ya kupata ufumbuzi ili waweze kujenga nyumba za walimu na uwanja wa michezo.

Wazee wa kimila wakifuatilia tukio katika mahafali hayo
Mgeni rasmi alihitimisha hotuba yake kwa kuwashukuru wananchi wote pamoja na Kamati ya Shule kwa kujumuika naye katika mahafali hayo, na pia kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura kwa chama tawala – CCM ili kuendelea kupata huduma nzuri za kijamii kwa sababu ndicho chama kinachounda serikali.
Kwa upande wake Mratibu Elimu Kata ya Nyanungu, Mwalimu Petro Nkoge Kimito, aliwataka wazazi kuepuka kuwaozesha watoto wa kike kabla ya kuhitimu masomo.
"Elimu ndiyo uti wa mgongo, msiozeshe hawa watoto, tunategemea wasome muwatunze na kuwashauri vizuri, tunategemea mambo makubwa,” alisema Mwalimu Kimito.

Wanafunzi wakitumbuiza kwa wimbo katika mahafali hayo. (Picha zote na Mara Online News)
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Getena, Philemon Allay, akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi, alisema: "Namshukuru sana mgeni rasmi Moses Makindi Jacob, tulimwalika na akakubali, nilimwambia nakualika nyumbani kwenu uje uongee na ufurahi na ndugu
zako.”
Aidha, Mwalimu Allay aliahidi kutunza vizuri kompyuta hiyo iweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuchochea maendeleo ya taaluma katika shule hiyo ya serikali iliyofunguliwa mwaka 2024 na kuchukua wanafunzi kutoka shule jirani katika kata ya Nyanungu.

No comments:
Post a Comment