NEWS

Tuesday, 28 October 2025

Watanzania kuamua kesho Jumatano Oktoba 29, 2025




Na Mwandishi Wetu

Watanzania zaidi ya milioni 30 walioandikishwa kupiga kura kesho Jumatano, Oktoba 29, 2025 wanatarajiwa kujitokeza kuchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani kwenye Uchaguzi Mkuu wa saba wa mfumo wa vyama vingi tangu nchi iingie kwenye mfumo huo mwaka 1992.

Tayari serikali imeshatangaza kwamba siku hiyo itakuwa ya mapumziko kwa wafanyakazi nchi nzima ili kuwapa fursa ya kuungana na Watanzania wengine katika uchaguzi huo unaofanyika kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.

Wagombea wa nafasi mbalimbali kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani wamehitimisha kampeni zao leo Jumanne na kusubiri uamuzi wa wananchi kutokana na kile walichokipanda kufuatia ahadi lukuki walizozitoa.

Wagombea wa nafasi ya urais kwa upande wa vyama vya upinzani zaidi ya 10 waliojitokeza kuwania nafasi hiyo watapambana na Rais wa sasa Dkt. Samia Suluhu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi kimekuwa kikipata ushindi kwa chaguzi zote zilizopita.

Kama wingi wa watu waliokuwa wakihudhuria mikutano ya kampeni ni kigezo sahihi cha ushindi, chama tawala - CCM bado kinatabiriwa kuwa na nafasi kubwa ya kuvibwaga vyama vya upinzani.

CCM, ambacho kiliundwa rasmi Februrari 5, 1977 kwa muungano wa vyama vya Afro-Shirazi Party na TANU kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, ni moja ya vyama vikongwe barani Afrika vinavyoendelea na utawala, kikiwemo chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini.

Sifa kubwa ya vyama vilivyozaa CCM ni kwamba viliendesha harakati za ukombozi za kupambana na wakoloni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages