
Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO) wa Tarime Rorya. SP Hamis Wembo, akizungumza na waendesha "bodaboda" wakati wa uzinduzi wa mafunzo yao kwa ufadhili wa Professor Mwera Foundation (PMF).
Tarime
-----------
Taasisi ya Professor Mwera (PMF) imejitolea kufadhili mafunzo maalum kwa waendesha pikipiki za abiria “bodaboda” zaidi ya 900 katika wilaya ya Tarime.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera, mafunzo hayo yatakuwa ya siku tatu mfululizo na yatagharimu shilingi zaidi ya milioni 90.
“Mafunzo hayo yatawajengea uwezo kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kuzingatia sharia za usalama wa barabarani,” Hezbon alisema katika hafla ya uzinduziwa mafunzo hayo jana kwenye Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa na PMF.

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera, akizungumza na waendesha bodaboda katika hafla ya uzinduzi wa mafunzo yao.

Mafunzo hayo yalizinduliwa na Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO) wa Tarime Rorya, SP Hamis Wembo, ambaye aliwataka bodaboda hao kuyazingatia ili yawezi kuwasaidia kufanya shughuli zao kwa usalama zaidi.
"Naomba tufanye kazi kwa malengo, tudundulize fedha kwa ajili ya kusoma na kupata leseni. Kupitia haya mafunzo tutajifunza mengi ili kupunguza ajali zisizo za lazima. Tunamshukuru sana Hezbon Peter Mwera kwa kufadhili mafunzo haya,” alisema RTO Wembo.
Wakizungumza katika uzinduzi huo, viongozi wa bodaboda hao walimshukuru Mkurugenzi Hezbon kwa kufadhili mafunzo hayo wakisema yatawasaidia kujua alama, sheria na taratibu za usalama barabarani.

Mwenyekiti wa Maafisa Usafirishaji "Bodaboda" Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Bhoke, akizungumza katika hafla hiyo.

Katibu wa Maofisa Wasafirishaji "Bodaboda" Halmashauri ya Mji wa Tarime, Dickson Christopher, akizungumza katika hafla hiyo.
Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinafundisha fani mbalimbali zikiwemo za ufundi magari, umeme, mabomba, uhazili, udereva, ushonaji, uongozaji watalii na upishi, miongoni mwa nyingine.
Mbali na chuo hicho cha ufundi, taasisi ya PMF inamiliki pia Shule ya Msingi Mwera Vision, Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko, Jogging Club, Mwera Jazz Band, PMF Restaurant.
No comments:
Post a Comment