NEWS

Tuesday, 11 November 2025

Muderspach Primary School yapata ufaulu wa kihistoria Mtihani wa Taifa Darasa la Saba 2025

Sehemu ya mabasi ya usafiri wa wanafunzi wa Muderspach Primary School
Na Mwandishi Wetu
Tarime
-----------

Ni katika eneo la Kibumaye, takriban kilomita tano kutoka mji wa Tarime, ndipo unaikuta Muderspach Primary School - shule ambayo imeweka historia mpya ya kung’ara kwa ufaulu bora katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba Mwaka 2025.

Matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) hivi karibuni, yanaonesha wanafunzi 53 wa shule hiyo wamepata ufaulu bora wa daraja la kwanza (A) na watano wamepata daraja la pili (B).

Ufaulu huo umeiwezesha shule hiyo yenye mchepuo wa Kiingereza kukaa kileleni na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya kati ya shule 33 kwenye kundi la idadi ya wanafunzi 40 na kuendelea.


Sehemu ya wanafunzi wa Muderspach Primary School waliofanya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba 2025.

Kwa upande mwingine, shule hiyo imeshika nafasi ya pili kwa ufaulu bora kati ya shule mama zote zinazomilikiwa na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Jimbo la Mara.

Akizungumza na Mara Online News ofisini leo, Mwalimu Mkuu wa Muderspach Primary School, Paul Basondole, ameeleza furaha waliyonayo kufuatia matokeo hayo ya heshima kubwa kwa shule hiyo.
Mwalimu Paul Masandola 
“Tumefurahi sana sisi kama watumishi - walimu pamoja na wazazi, wanafunzi na wadau wa shule, wakiwemo viongozi wetu wa Kanisa kuona kazi tuliyofanya kwa bidii imezaa matunda mazuri,” amesema Mwl. Basondole.

Siri ya mafanikio
Kwa mujibu wa Mwl. Basondole, mafanikio ya shule yake katika mtihani huo ni matokeo ya kuchapa kazi na kujituma kwa walimu na wanafunzi katika masomo.

“Tulihakikisha tunamaliza mada zote za masomo kwa wakati, tukafanya mazoezi ya kutosha na walimu wetu wakafanya juhudi kubwa kuhakikisha hakuna mwanafunzi aliyebaki nyuma,” amesema.

Zaidi ya hayo, Basondole amesema walimu walifuata njia bora na shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji kwa vitendo, jambo lililowasaidia wanafunzi kuelewa kwa undani na kujenga ujasiri wa kujibu mitihani kwa umahiri.


Moja ya majengo ya Muderspach Primary School

Mwalimu Mkuu wa Muderspach Primary School pia anaelekeza pongezi za dhati kwa wazazi na jamii nzima kwa mchango wao mkubwa kwenye safari ya mafanikio hayo.

“Wazazi wamekuwa na uhusiano mzuri na walimu, wanawapa motisha na kulipa ada za wanafunzi kwa wakati. Mfano, mwaka jana walileta mbuzi kama zawadi ya pongezi kwa walimu,” amesema Mwl. Basondole.

Upekee wa Muderspach
Wakati shule nyingi zikilenga tu matokeo ya darasani, Muderspach Primary School imejijengea utambulisho wa kipekee kwa kumtanguliza Mungu na msisitizo wa bidii ya walimu na usimamizi wa karibu kwa wanafunzi.

“Tunamfanya Mungu kuwa wa kwanza. Walimu wetu wanafanya kazi kwa bidii, tunasimamia wanafunzi kwa karibu, tunafundisha kwa vitendo na tunawapeleka wanafunzi katika ziara za mafunzo, ikiwemo kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti na sehemu nyingine.


Wanafunzi wakiwa kwenye gwaride ndani ya Muderspach Primary School

“Shule yetu pia imewekeza kwenye miundombinu ya uhakika, ikiwemo huduma bora za afya zinazopatikana kwenye zahanati ya shule, maji safi na salama pamoja na lishe bora kwa wanafunzi wetu.

“Vilevile, shule yetu ina maabara ya kompyuta na vifaa vyote vya kufundishia na kujifunzia, mazingira rafiki ya kusoma pamoja na usafiri bora na wa uhakika kwa wanafunzi wa kutwa,” ameeleza Mwl. Basondole.


Wanafunzi wa Muderspach Primary School wakiwa katika darasa la kompyuta

Hivyo, Mwl. Basondole amewaomba wazazi na wadau mbalimbali kuendelea kuiamini Muderspach Primary School kwani ni miongoni mwa shule chache zinazofundisha maarifa ya kumjua Mungu na elimu dunia kwa viwango vya juu.

Mikakati ya kudumisha ufaulu
Uongozi wa Muderspach Primary School umeweka mikakati thabiti kuhakikisha kuwa kiwango cha ufaulu hakishuki bali kinaimarika zaidi.

“Tunaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu, ikiwemo kulipa mishahara kwa wakati na kuwapa makazi bora, lakini pia motisha hadi kwa watumishi wasio walimu pamoja na wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani na nidhamu,” amesema Mwl. Basondole.


Wanafunzi ndani ya Muderspach Primary School

Kuhusu wanafunzi wa Muderspach Primary School waliofaulu mtihani huo wa kuhitimu elimu ya msingi, Mwl. Basondole anawashauri kutoridhika na hatua hiyo bali waongeze bidii katika masomo na kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo.

“Ufaulu huu usiwe mwisho, bali mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio. Tunataka wawe mabalozi wazuri wa shule yetu popote waendapo,” amesema.

Dira ya baadaye
Kimsingi, Muderspach Primary School haijaridhika na mafanikio hayo ya ufaulu bora. Mwl. Basondole anasema bado wana ndoto kubwa za kuendelea kupaa katika nyanja za elimu.

“Tunapanga kuanza kufundisha lugha ya Kichina, kuanzisha shule ya sekondari, kuongeza magari na kuweka kamera za CCTV kwenye mabweni, madarasa na maeneo mengine muhimu ya shule yetu,” amebainisha Mwalimu Mkuu huyo.

Kwa ujumla, Muderspach Primary School imeonesha kuwa mafanikio ya kielimu hayaji kwa bahati, bali ni matokeo ya imani ya kiroho, juhudi, ushirikiano, bidii, ubunifu, uaminifu na nidhamu.
Picha ya pamoja wakati wa Mahafali ya Darasa la Saba 2025 ya Mudespach Primary School hivi karibuni
Kwa falsafa yake ya “Mungu Kwanza”, Muderspach Primary School imejipambanua kuwa taa ya maarifa na maadili katika wilaya ya Tarime kama si mkoa wa Mara.

#Wasiliana na Muderspach Primary School kwa namba: 0787249162
Read Also Section Example





No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages