NEWS

Wednesday, 3 December 2025

DPP afuta mashtaka ya uhaini dhidi ya Niffer, Chavala, mahakama yawaachia huru




Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
------------------

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Polisi nchini (DPP), imewafutia mashtaka ya uhaini na uchochezi mfanyabiashara Jennifer Jovin - maarufu Niffer, na Mika Chavala, waliokamatwa kutokana na vurugu za Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka mkuu.

Hatua hiyo imekuja wakati Tume ya Uchunguzi wa vurugu hizo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiendelea na kazi hiyo.

Ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa wamefurika katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Jumatano Desemba 3, 2025 walilipuka kwa vilio vya furaha wakati ilipotangazwa kuwa wawili hao wameachiwa huru.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya DPP kuwasilisha ombi mahakamani la kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi dhidi ya Niffer na Chavala, ambapo Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamua, alikubaliana na ombi hilo la upande wa Jamhuri na kutangaza rasmi kuwaachia huru.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka gerezani, Niffer aliishukuru familia yake, mamlaka mbalimbali na Rais Samia, akisema bado anaendelea kuelewa kilichotokea lakini anafurahi kuachiwa huru.

Wawili hao walikuwa wanakabiliwa na kesi namba 26388/2025 chini ya kifungu cha 92(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20, marejeo ya mwaka 2023, wakihusishwa na vurugu za maandamano wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Kwa upande wake Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alisema DPP ametumia madaraka yake ipasavyo na kwamba hatua hiyo imefungua ukurasa mpya, ingawa sheria haimlazimishi kueleza sababu za kufuta mashtaka hayo.

Wachambuzi wa masuala ya sheria wamesema uamuzi wa kuwafutia mashtaka unaonesha mabadiliko katika namna mamlaka zinavyochukulia kesi za uhaini.

Ripoti zinaonesha kuwa kati ya Novemba 10 na 11, 2025, watu zaidi ya 600 walikamatwa nchini na kusomewa mashtaka ya uhaini katika mahakama mbalimbali kutokana na vurugu za maandamano zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages