
Mwenyekiti mpya wa ALAT Mkoa wa Mara, Ayub Mwita Makuruma,
Musoma
----------------
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Mwita Makuruma amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Mara.
Makuruma aliibuka na ushindi huo kwa kupata kura 20 kati ya 39 katika mkutano wa ALAT uliofanyika mjini Musoma jana Machi 4, 2026, huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati, akishinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti Makuruma aliwashukuru wajumbe na kusisitiza ushirikiano na nidhamu katika utendaji kazi kwa maslahi ya mkoa wa Mara.
Aidha, aliwakumbusha madiwani kusimamia ukusanyaji na usimamizi wa mapato katika halmashauri zao.

Mwenyekiti Makuruma akizungumza mara baada ya kuchaguliwa
"Ninawashukuru kwa kuniamini… hakuna aliyeshinda, wote tumeshinda, yapo mengi ambayo napaswa kuyasimamia, ikiwemo maslahi ya madiwani na Mheshimiwa Rais aliahidi kuyafanyia kazi.
"Chombo hiki cha ALAT kituunganishe pamoja, umoja ni muhimu sana katika kusonga mbele, nia ya dhati ni kujenga Mara, lazima tukashirikiane, tuheshimiane tuelewe kuwa tunajenga nyumba moja.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata maendeleo, na ndiyo matarajio ya wote waliotuchagua, wanatarajia kuona kuna hatua imepigwa katika maeneo yao.
"Kuna fedha nyingi ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akizitoa katika serikali za mitaa na changamoto imekuwa ni usimamizi,”alisema Mwenyekiti Makuruma na kuendelea:
“Niwaombe kila mtu twende tukiwa tumeshikamana kuhakikisha kuwa tunasimamia mapato kukusanywa vizuri, kuhakikisha kwamba fedha ambazo zinakwenda katika miradi ya maendeleo zinasimamiwa vizuri kwa maana ya mapato ya ndani na serikali kuu."

Mwenyekiti Makuruma (wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) na wajumbe wengine wa ALAT Mkoa wa Mara wakifurahia jambo kabla ya uchaguzi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, alichaguliwa kwa kura zote 39 kuwa Mwakilishi wa ALAT Taifa, huku Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji, pia akichaguliwa kwa kura zote 39 kuwa Mwakilishi wa Wabunge kwenye ALAT Mkoa wa Mara.
Miongoni mwa majukumu ya ALAT ni kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha ‘value for money’ na kila halmashauri inapata maendeleo bila kubaki nyuma.
Ni chombo ambacho huwakutanisha wenyeviti na wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa, pamoja na madiwani wengine wanaoteuliwa kuwa wajumbe wa jumuiya hiyo.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment