NEWS

Tuesday, 2 December 2025

Tarime: Chifu wa Watimbaru Peter Zacharia aomba vijana kuepuka vishawishi vya kuvuruga amani



Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zacharia (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali kijijini Nkongore, Tarime leo Desemba 2, 2025.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------

Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zacharia, ametoa wito wa kuwaomba vijana kuwa na msimamo wa kulinda amani ya nchi na kuepuka vishawishi vya uchochezi na vurugu.

Chifu Zakaria ametoa wito huo alipokutana na baadhi ya viongozi wengine wa koo hiyo pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, kijijini Nkongole, leo Desemba 2, 2025.


Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, akisalimiana na Chifu Zakaria. Katikati ni Katibu wa Chifu huyo, Justin Manga.

"Sisi kama viongozi wa kimila tunataka amani ili wananchi wetu wakae kwa usalama, kwa sababu vurugu zilizotokea zilitufanya tuwe kama wafungwa. Tunaendelea kuwasihi vijana wetu wasifanye vurugu kwa kufuata mkumbo na kuhatarisha amani na usalama wa nchi yetu," amesema.

Ameongeza: "Sisi tayari tumewatangazia wananchi wetu kwamba hatutaki mambo ya maandamano na wao wameonesha kukubaliana nasi kwamba maandamano yanaleta hasara katika taifa."


Katibu wa Chifu Zakaria, Justin Manga, akizungumza katika kikao hicho.

Katika hatua nyingine, viongozi hao wamejadili mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya Tarime, ambapo Chifu Zacharia ametumia nafasi hiyo kumuomba Mbunge Matiko kufikisha kwa Serikali Kuu ombi la ujenzi wa chuo kikuu katika mji wa Tarime.

"Kwa kuwa Tarime ni wilaya kubwa na kongwe, tunaomba serikali itusaidie kutupa chuo kikuu ili wanafunzi wetu na majirani wasipate shida ya kwenda mikoa ya mbali kama Mbeya na Dar es salaam kufuata masomo," amesema Chief Zacharia.

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, amewashukuru viongozi hao kwa kujali na kuzingatia amani ya nchi na kuahidi kufikisha maombi yao Serikali Kuu ili yafanyiwe kazi zaidi.

"Nitoe shukuruni zangu kwenu kwa juhudi zenu za kuhakikisha kwamba Tarime inaendelea kuwa ni mji wenye amani, lakini pia nitoe ahadi kwamba yote mliyoomba kama ujenzi wa chuo kikuu nitayafikisha serikalini na nitasema kwamba tuna eneo kubwa linalotosha kabisa ujenzi wa chuo hicho," amesema Matiko.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Katibu wa Wazee wa Kimila Wilaya ya Tarime, Mwita Nyasibora na Mwenyekiti wa Koo ya Watimbaru, Charles Mwita Mkogogo.


Katibu wa Wazee wa Kimila Wilaya ya Tarime, Mwita Nyasibora.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages