
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na baadhi ya wazee wa jijini Dar es Salaam (hawapo picha), leo Desemba 2, 2025.
Dar es Salaam
-------------------
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali yake iko tayari kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ya jamii, ili kuondoa mapungufu yaliyopo na kuimarisha amani na usalama nchini.
Amesema jeraha lililotokana na vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 2025, litatibiwa na Watanzania wenyewe kupitia majukwaa ya mazungumzo, ushirikiano wa wanasiasa, wazee na kuwashauri vijana kutojiingiza kwenye mipango ya vurugu.
“Tukae tuzungumze. Wazee wetu na vijana wetu wasitumike. Tanzania itajengwa na Watanzania,” amesema Rais Samia katika sehemu ya hotuba yake alipokutana na kuzungumza na baadhi ya wazee wa jijini Dar es Salaam, leo Desemba 2, 2025.

Sehemu ya wazee wa jijini Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Rais Samia
“Yaliyopita si ndwele tuganje yajayo… Kwa hiyo na sisi hatuna budi kukaa - kuzungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo… wanadamu hukosana - wakaelewana,” amesema na kuendelea:
“Hatusemi serikali labda tuko safi - hatuna makosa, hapana. Inawezekana kabisa kuna mapungufu, na hakuna serikali yoyote isiyo na mapungufu, lakini wanakaa wanazungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo.”
Kwa upande mwingine, Rais Samia amezikosoa taasisi za dini zilizojiingiza kwenye mkumbo wa mijadala na matamko yanayochochea mgawanyiko wa Watanzania.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kusimama katika mstari sahihi, kwa kuwa mamlaka yote yametoka kwa Mungu, bila kujali kama kiongozi ni mwanamke au mwanamume.
“Viongozi wa dini msijivishe majoho ya kuonesha kuwa mnaweza ku- override madhehebu mengine,” ameonya.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa nchi amesema serikali yake itaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda amani na usalama wa nchi, ikiwemo kuhakikisha siasa za ushindani zinakwenda kwa mujibu wa sheria bila kuruhusu mipango ya vurugu.
Hivyo, ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi kuwa watulivu, wenye busara na kulinda amani ya nchi kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Kwa upande wao, wazee hao akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Dar es Salaam, Salumu Matimbwa, pamoja na mambo mengine, wamempongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuanzisha wizara maalum ya kushughulikia masuala ya vijana nchini.
Pia, wamemshukuru Rais Samia kwa maelekezo yake ya kuwapatia wazee bima ya afya ndani ya siku 10 za kwanza za uongozi wake baada ya kuapisha, wakisema hatua hiyo itakuwa faraja kubwa kwa kundi hilo la jamii.
No comments:
Post a Comment