
Sehemu ya miche bora imeyozalishwa na WAMACU kwa ajili ya kupanua kilimo cha kahawa mkoani Mara
Na Mwandishi Wetu
Mara
---------
Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kimebania kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa hadi kufikia tani 15,000 ifikapo mwaka 2030, Meneja Mkuu (GM) wa ushirika huo, Samwel Marwa Gisiboye, amesema.
Ili kufikia lengo hilo ambalo ni la kimkoa, tayari WAMACU wameanza kufanya uwekezaji mkubwa wa kuzalisha miche bora ya kahawa aina ya chotara, kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima katika wilaya za Tarime, Serengeti, Butiama na Rorya zinazolima zao hilo la biashara.
GM Gisiboye anasema shughuli ya kusambaza miche hiyo inatarajiwa kufanyika kwa miezi mitatu hadi minne kutegemeana na majira ya mvua.
“Tayari tumezalisha miche laki tano na imeanza kwenda kwa wakulima,” GM Gisiboye alieleza katika mahojiano maalum na Mara Nonline News ofisini kwake mjini Tarime, hivi karibuni.
Alisema miche hiyo mbali na kuwa na uwezo wa kutoa mavuno makubwa, haishambuliwi na magonjwa ya zao hilo.
“Mche mmoja una uwezo wa kutoa kilo tatu hadi tano kwa msimu - tofauti na ya zamani ambayo ilikuwa inatoa nusu kilo,” anasema matalamu wa masuala ya kahawa katoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Kwa mujibu wa GM Gisiboye, mkulima hulipia kila mche shilingi 300 ili kuchangia gharama za uendelezaji mradi na nauli ya usafiri wa kumfikishia miche yake alipo.
Uchangiaji huo wa gharama unamfanya mkulima kujiona mmiliki wa miche hiyo, hivyo kuithamini na kuitunza kwa mustakabali mwema wa uchumi wake.

Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Marwa Gisiboye.
WAMACU inasema uzalishaji wa kahawa kwa sasa unakimbilia tani 3,000 kwa mwaka na kwamba lengo la mkoa ni kuzalisha tani 15,000 za kahawa ambayo inauzwa katika soko la dunia ifikapo mwaka 2030.
Kahawa inayozalishwa na WAMACU inatajwa kufanya vizuri katika soko la dunia kutokana na uwepo wa ardhi ambayo ni rafiki wa zao hilo mkoani Mara.
Hadi sasa, wilaya ya Tarime inaongaza kwa kuzalisha kahawa aina ya Arabica, ambayo inatamba katika soko la dunia.
Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU, Momanyi Range, anajivunia mradi huo wa kuzalisha miche bora akisema utakuwa na tija kubwa kwa maendeleo ya sekta ya kahawa katika mkoa huo.
“Miche hii itaongeza mashamba ya kahawa, uzalishaji utaongezeka. Wito wangu kwa wakulima ni kwamba wajitokeze wachukue miche ambayo ni bora kwa bei nafuu wakapande,” anasema Momanyi.
Kwa upande wake mkulima wa kahawa kutoka kata ya Ketare wilayani Tarime, Peter Keba Wangwe, ameeleza kufurahia mradi huo akisema tayari ameshanunua na kupanda mamia ya miche hiyo.
“Tunaishukuru WAMACU kwa kusimamia vizuri mradi huu, miche wanayozalisha ina afya, na tayari nimechukua na kuipanda, na ninashukuru mvua imeanza kunyesha” anasema Keba.
Aidha, mkulima huyo anaupongeza ushirika huo kwa kuanzisha utaratibu wa kuwataka wakulima kuchagia gharama za miche hiyo.
“Kitu nilichopenda, WAMACU hawatoi bure hii miche, maana miaka ya nyuma baadhi ya wakulima walikuwa wanachukua bure na kuitekeleza, lakini kwa kuchangia gharama kila mmoja ataithamini na kuitunza vizuri.
“Kuhusu soko, naona wanakusanya kahawa kwa bei nzuri - shilingi 4,500 kwa kilo moja, na tuna matumaini kwamba itazidi kupanda, hivyo wakulima tutaongeza kipato,” anasema Keba.

Naye Augustino Mrimi, mkulima wa kahawa kutoka kata ya Binagi, Tarime anasema: “Mimi tayari nimeshanunua miche 200 na nina mpango wa kuongeza miche 1,000.”
Kadri wakulima wanavyochangamkia uchukuaji wa miche hiyo, ndivyo ndoto ya mkoa wa Mara ya kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa kahawa nchini inavyokaribia kutimia.
Sambamba na hilo, mradi wa uzalishaji wa miche hiyo ya kahawa unatarajiwa kuongeza uzalishaji zaidi wa zao hilo na kulisha kiwanda cha kuchakata kahawa kinachomilikiwa na WAMACU Ltd - kilichopo mjini Tarime.
Wadau wanaoshirikiana na WAMACU kutekeleza mradi wa uzalishaji miche bora - wenye thamani ya milioni 115, ni Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), wataalamu wa kilimo kutoka Halmashauri za Wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
GM Gisiboye anasema TADB imechochea maendeleo ya zao la kahawa mkoani Mara kupitia WAMACU, hasa katika ununuzi wa mitambo ya kubangua kahawa kavu na mbivu, dhamana na mkopo wa miche kwa awamu ya kwanza.

Hadi sasa, WAMACU ina Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS) 32 ambavyo vinajishughulisha na uzalishaji wa zao la kahawa.
Ushirika wa WAMACU Ltd una leseni ya kuuza kahawa nje ya nchi kama vile Uingereza na Marekani, baada ya kuikusanya kutoka kwa wakulima kupitia AMCOS na kuiongezea thamani.

Pia, WAMACU Ltd ni miongoni mwa vyama vikuu vya ushirika vilivyopewa kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku ya serikali kwa wakulima kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), TFC na OCP.
Aidha, kwa sasa ushirika huo una leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
No comments:
Post a Comment