NEWS

Saturday, 6 December 2025

Tarime Mji: Shule ya Mwera Vision yasherehekea Mahafali ya Tano ya Darasa la Awali



Picha ya pamoja ya mgeni rasmi, viongozi, walimu na wanafunzi wakati wa Mahafali ya Tano ya Darasa la Awali ya Shule ya Awali na Msingi Mwera Vision.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-----------

Shule ya Awali na Msingi ya Mwera Vision yenye mchepuo wa Kiingereza iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime, mkoani Mara, imesherehekea Mahafali ya Tano ya Darasa la Awali, huku ikipongezwa kwa kufanya vizuri kitaaluma.

Mahafali hayo ya wanafunzi 20 (wavulana 10 na wasichana 10), yalifanyika Desemba 3, 2025 katika viwanja vya shule hiyo inayomilikiwa na Taasisi ya Professor Mwera (PMF).


Picha ya pamoja ya wazazi na wahitimu hao wa darasa la awali

Akizungumza katika mahafali hayo, mgeni rasmi, Afisa Elimu Kata ya Rebu, Mwl. Imani Hamza Buchafwe, aliipongeza shule hiyo kwa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wake anajua Kusoma, Kuhesabu na Kuandika (KKK).

"Nimekuwa mdau wa shule hii na naitembelea sana kuangalia mazingira ya usomaji, kwa kweli walimu wanajitahidi sana, hakuna mwanafunzi asiyejua KKK, watoto hapa wanaiva ninaomba wazazi mturudishie hao wanafunzi waendelee na darasa la kwanza hapa” alisema Mwl. Imani.

Pia, aliipongeza Taasisi ya PMF ushirikiano wake kwa serikali, pamoja na kuzingatia maelekezo ya vyakula vinavyohitajika kwa wanafunzi wa shule hiyo.


Mwl. Imani akizungumza katika mahafali hayo. Kushoto ni MKurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera.


Mgeni rasmi Mwl. Imani akikabidhi vyeti kwa wanafunzi hao

Kwa upande wake Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera, alitumia fursa hiyo kutangaza ofa ya kwa wanafunzi watakaoendelea kusoma shuleni hapo hadi darasa la saba, kwamba watasoma bure katika Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko ambayo pia inamilikiwa na taasisi hiyo.

"Watakaosoma hapa tangu mwanzo na kujiunga na Sekondari ya Tarime Mchanganyiko tutawasomesha bure,” alisema Hezbon na kuendelea:

"Na kwa kuwa tuna chuo cha mafunzo ya ufundi hapa, tunaenda kuwapa ofa ya kununua laptop (kompyuta mpakato) kwa shilingi laki moja na nusu kwa kila mtoto, pamoja kusoma fani moja ya ufundi bila kusahau lugha mbili za kigeni - Kichina na Kifaransa."


Mkurugenzi Hezbon akizungumza katika mahafali hayo


Taasisi ya PMF pia inamiliki Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime (TVTC) ambacho kinafundisha fani mbalimbali, zikiwemo za ufundi magari, umeme, mabomba, uhazili, udereva, ushonaji, uongozaji watalii na upishi, miongoni mwa nyingine.

Mbali na chuo hicho cha TVTC, Shule ya Sekondari Tarime Mchanganyiko na Shule ya Awali na Msingi Mwera Vision, Taasisi ya PMF inamiliki pia Jogging Club, Mwera Jazz Band na PMF Restaurant.


Wahitimu wa darasa la awali wakati wa mahafali yao


Viongozi, walimu na wahitimu wa darasa la awali wakati wa mahafali hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages