
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma, akihutubia kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
Mkoa wa Mara upo kwenye hatua ya kuelekea kupata uongozi wa serikali za mitaa, ambapo Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika mkoa huo inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti wake mpya siku chache zijazo.
Jina linaloendelea kutawala midomo ya wadau wa siasa na maendeleo kuelekea uchaguzi huo ni Ayub Mwita Makuruma ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe, umaarufu wake wa kisiasa ulianza kujengeka kwa kasi mwaka 2020 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo - nafasi nyeti inayohitaji busara, uadilifu na uwezo wa kusimamia rasilimali za umma.
Uchaguzi ujao wa Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara unavuta hisia za wadau wengi kutokana na kuhitaji kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia maslahi ya wananchi, rasilimali za umma na ushirikiano wa halmashauri.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa kisiasa na maoni ya viongozi wa halmashauri mbalimbali mkoani Mara, Makuruma anaingia kwenye kinyang’anyiro hicho akiwa na uzoefu, rekodi ya utendaji na mtaji wa uongozi unaomfanya aonekane chaguo sahihi zaidi la kuiongoza ALAT Mkoa wa Mara kwa miaka mitano ijayo.
Makuruma anaelezewa na watu wengi kama kiongozi mpole, mnyenyekevu, msikivu na mchapakazi - sifa ambazo ni nadra kuzipata kwa wakati mmoja katika uongozi wa umma.
Chini ya uenyekiti wa Makuruma, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imeshuhudia maboresho makubwa katika sekta za afya, elimu na huduma za jamii, sambamba na kuimarika kwa usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Lakini kilichoifanya halmashauri hiyo itajwe kama mfano wa kuigwa ni ongezeko la mapato ya ndani, ambayo yameripotiwa kufikia shilingi bilioni 6.6 kutokana na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na usimamizi mzuri.
Hilo ni jambo linaloipa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti uwezo mkubwa wa kujitegemea na kutekeleza miradi yake bila kutegemea sana ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Kitendo cha Makuruma kushinda tena udiwani wa Busawe katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kisha kuchaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, ni hatua inayotafsiriwa kisiasa kama kura ya imani kutoka kwa wananchi na madiwani wenzake.
Moja ya hoja nzito zaidi zinazombeba Makuruma ni uzoefu wake wa kipekee ndani ya ALAT, kwani tofauti na wenyeviti wengine wa halmashauri mkoani Mara, ndiye Mwenyekiti pekee aliyerejea madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, hali inayomfanya awe mjumbe mwenye uzoefu mkubwa ndani ya jumuiya hiyo.
Katika mazingira ambayo karibu wenyeviti wote wa halmashauri za mkoani Mara ni wapya baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita, Makuruma anajitokeza kama mjumbe mzoefu wa ALAT. Hiyo ni faida isiyopingika, hasa katika kipindi hiki ambacho jumuiya hiyo inahitaji uthabiti.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara, Daniel Komote kutoka Halmashauri ya Mji wa Tarime safari hii hayupo kwenye mtandao wa wenyeviti wa halmashauri - baada ya kushindwa kutetea udiwani wake katika kata ya Nkende.
Katika siasa, ombwe la uongozi hujazwa na mhusika mwenye mtaji mkubwa wa uzoefu, na katika hilo, Makuruma ndiye anaonekana kumiliki mtaji huo ndani ya ALAT Mkoa wa Mara.
Makuruma anatajwa kuwa na mahusiano mazuri na madiwani, watendaji wa halmashauri, wananchi na wadau wa maendeleo. Tukio la Umoja wa Makatibu wa CCM Wilaya ya Serengeti kumpa zawadi ya ng’ombe na cheti cha pongezi wiki hii, ni ishara ya mtaji wa kijamii na kisiasa alionao.
Kwa jumla, nafasi ya Ayub Mwita Makuruma katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara ni kubwa, kwani anabeba uzoefu kwenye jumuia hiyo, rekodi ya utendaji, uthabiti wa uongozi na uwezo wa kutetea maslahi ya halmashauri.
Naam, katika mazingira ambayo ALAT inahitaji kiongozi anayeweza kuunganisha sauti za halmashauri, kusukuma ajenda za ugatuaji wa madaraka na kujenga ushawishi wa serikali za mitaa, jina la Makuruma linaendelea kutajwa kuwa na nafasi kubwa.
Kwa ujumla, wachambuzi wa siasa za mitaa wanaona kuwa Makuruma anaingia kwenye uchaguzi wa Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mara akiwa na faida tatu kuu; uzoefu wa ndani wa jumuiya, rekodi thabiti ya maendeleo na uwezo wa kuunganisha wadau.
Kwa muktadha huo, si ajabu jina la Ayub Mwita Makuruma kuendelea kutajwa kama mgombea ajaye mwenye nafasi kubwa zaidi ya kuibuka Mwenyekiti mpya wa ALAT Mkoa wa Mara - nafasi inayohitaji kiongozi mwenye maono, uzoefu na uthubutu wa kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya serikali za mitaa.
Majukumu ya ALAT
Miongoni mwa majukumu ya ALAT ni kusimamia miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha ‘value for money’ na kila halmashauri inapata maendeleo bila kubaki nyuma.
Ni chombo ambacho huwakutanisha wenyeviti na wakurugenzi wote wa halmashauri za mkoa, pamoja na madiwani wengine wanaoteuliwa kuwa wajumbe wa jumuiya hiyo.
No comments:
Post a Comment