
Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa.
Mara Online News
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewaruhusu wanafunzi waliofeli katika mitihani ya kidato cha pili kuendelea na kidato cha tatu badala ya kurudia kidato cha pili kama ambavyo imekuwa ikifanyika nchini.
Hata hivyo, wizara imeelekeza kwamba wanafunzi hao watapewa programu maalum huku wakiendelea na masomo ya kidato cha tatu.
Hatua hiyo ilitangazwa na Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa, jana Januari 10, 2026 saa chache baada ya Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) kutangaza matokeo ya mitihani ya upimaji wa kidato cha pili na darasa la nne ya mwaka 2025.
Kwa mara ya kwanza, mtihani wa kidato cha pili mwaka 2025 ulifanyika katika mikondo miwili - ukihusisha mkondo wa amali, ambapo matokeo yanaonesha wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 100 masomo ya fani za amali za uhandisi, umeme, mitambo, magari na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Pia, katika masomo ya fani za amali zisizo za uhandisi, zikiwemo za kilimo na chakula, ukarimu na utalii, mavazi na ushonaji, michezo na sanaa za ubunifu; wanafunzi wamefaulu kwa asilimia 100 masomo manane kati ya 14.
Katika taarifa yake kwa umma, Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene, alisema “Ninaelekeza kwamba wanafunzi ambao hawakufikia alama za ufaulu za kidato cha pili mwaka 2025 waendelee na kidato cha tatu badala ya kukariri (kurudia) kidato cha pili.”
Kamishna Lyabwene aliendelea “Wanafunzi hao watapewa programu maalum rekebishi (remedial programme) itakayotolewa wakati wakiendelea na masomo yao ya kidato cha tatu.”
Alisema uamuzi huo wa serikali umezingatia kwamba mitaala iliyoboreshwa inatekelezwa kwa awamu, na wanafunzi waliofanya mtihani wa upimaji wa kidato cha pili mwaka 2025 walitumia mtaala wa zamani na watamaliza kidato cha nne kwa kutumia mtaala huo huo.
“Wanafunzi wanaoingia kidato cha pili mwaka 2026 watatumia mtaala ulioboreshwa ambao walianza kuutumia kidato cha kwanza, hivyo endapo walioshindwa kufikia alama za ufaulu watarudia kidato cha pili watalazimika kutumia mtaala ulioboreshwa ambao hawakuanza nao kidato cha kwanza. Hii italeta changamoto kubwa katika ujifunzaji na ufundishaji,” alifafanua.
“Ni matarajio yetu kuwa wakuu wa shule zenye wanafunzi husika watatekeleza maelekezo haya kwa ukamilifu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanafundishwa na kujifunza ipasavyo ili kupata umahiri uliokusudiwa,” Kamishna Lyabwene alisisitiza katika taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment