NEWS

Friday, 30 January 2026

TRA Mara yatoa mafunzo ya IDRAS kwa walipakodi



Afisa Msimamizi wa Kodi, Rebeca Hezron, akizungumza kwenye mafunzo ya mfumo wa IDRAS yaliandaliwa na TRA Mkoa wa Mara kwa walipakodi mjini Musoma jana.

Na Godfrey Marwa
Musoma
---------------

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imetoa mafunzo ya mfumo mpya wa ulipaji kodi ujulikanayo kama IDRAS kwa walipakodi na wafanyabiashara wa mkoa huo.

Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Nassoro Ndemo, alizindua mafunzo hayo katika semina maalumu iliyofanyika kwenye Hotel ya MK, mjini Musoma, jana Januari 30, 2026.

"IDRAS ni mfumo wa kusimamia kodi za ndani, watu wote - wafanyabiashara, walipakodi na wasiofanya biashara, yeyote ambaye ana miaka 18 anatakiwa kisheria kuwa na TIN ( Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi),” Ndemo aliwambia washiriki wa mafunzo hayo.

"Mtu ambaye hafanyi biashara anaweza kuwa anataka leseni ya kuendesha chombo cha moto au kumiliki pikipiki au gari lazima awe na Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi, anahitaji kujua mfumo huu ili anapohitaji huduma aweze kuingia bila shida yoyote,” alifafanua.


Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Nassoro Ndemo.

Mfumo huo wa IDRAS utakaotumika kusimamia na kukusanya kodi za ndani nchini utaanza kutumika Februari 9, 2026.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara na walipakodi kuufahamu na kuutumia mfumo huo kwa kuwa na dirisha moja katika usimamiaji na ulipaji kodi kwa njia ya mtandao, hali ambayo itapunguza malalamiko yatokanayo na mfumo uliopo.


Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada

Kwa upande wake Afisa Msimamizi wa Kodi, Rebeca Hezron, alitaja faida za mfumo wa IDRAS mbele ya washiriki wa semina hiyo.

"Mfumo huu umekuja na mapinduzi makuu matatu, huduma zote zitapatikana kwa njia ya mtandao, hautatakiwa kusafiri kutoka huko ulipo mpaka ofisini, chochote utakachotaka kuuliza ndani ya TRA utakipata kupitia mtandao siku saba za wiki saa 24,” alisema Rebecca.

Alisema mfumo wa IDRAS utarahisisha zaidi huduma kwa walipakodi. “Unaweza kutengeneza 'clearance' kupitia mfumo wa IDRAS, na wafanyabiashara na walipakodi wanaweza kutoa risiti kwa njia ya mtandao bila mashine ya EFD.” Aliongeza.


Sehemu nyingine ya washiriki wakifuatilia mada

Washiriki wa mafunzo hayo walisema ujio wa mfumo huo utakuwa suluhisho kwa changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo.

"Tumefurahia na ujio mpya wa mfumo wa IDRAS, kwani sisi kama walipakodi utakuwa umetusaidia katika ku- submit returns zetu zote kwa urahisi.

“Tulikuwa tukikabiliwa na changamoto hasa unapokuwa umepata huduma kwa mtu ambaye ni 'foreigner', mfumo utatusaidia kusajili na kuwa na TIN zao na kuweza ku- submit malipo yao kikamilifu," alisema Thresia Alyoce Massawe, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.

Mshiriki mwingine aliyejitabulisha kwa jina la Timas Nyantora, alisema: ”Huu mfumo wa IDRAS utasaidia nchi yetu kupata maendeleo, tumeletewa huduma mpaka ndani, wafanyabiashara ambao ni waoga watalipa kodi kwa uhuru bila urasimu.”

IDRAS (Intergrated Domestic Revenue Administration System) ni Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani unaolenga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidigitali kwenye huduma za kikodi nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages