NEWS

Friday, 2 January 2026

Uwekezaji: GBP yafungua kituo cha mafuta Butiama, RC Mara ahimiza ushirikiano kwa wawekezaji



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (aliyevaa suti), Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika (wa pili kulia), Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Mahera (kulia), wakiwa na wafanyakazi wa GBP wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafuta cha kampuni hiyo katika eneo la Makutano ya Juu wilayani Butiama.

Na Mwandishi Wetu
Butiama
-------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amezindua kituo cha mafuta cha GBP katika eneo la Makutano ya Juu wilayani Butiama na kuwaomba wananchi wa mkoa huo kuwapa wawekezaji ushirikiano.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Januari 1, 2026, RC Mtambi alisema wawekezaji wana faida kubwa kwa jamii inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na kuisogezea bidhaa na huduma jirani, hivyo kutolazimika kufuata huduma hizo mbali na kwa gharama kubwa.

“Kwa mfano kituo hiki cha mafuta kisingekuwepo mngelazimika kufuata mafuta mbali, jambo ambalo lingewaongezea gharama, lakini pia kimetoa ajira kwa vijana wa mkoa wa Mara na Butiama,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwakemea wanaoharibu mali za wawekezaji kwani uwekezaji una manufaa kwa jamii husika.

RC Mtambi, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha mafuta cha GBP katika eneo la Makutano ya Juu wilayani Butiama.

Aidha, RC Mtambia aliwakumbusha wananchi kutambua kuwa suala la ulinzi wa nchi ni jukumu la wananchi wote, na vyombo vya ulinzi vina jukumu la kutoa uongozi na utaalamu kuhusiana na namna bora ya kulinda nchi.

Aliwataka wananchi, hususan maafisa usafirishaji kuacha kutumika na watu wabaya kuharibu miundombinu iliyojengwa katika maeneo yao.

Alisema uwekezaji wa Kampuni ya GBP hapa nchini unatokana na sheria na sera nzuri za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo vinavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

RC Mtambi aliipongeza kampuni hiyo kwa kuwekeza katika mkoa wa Mara, na kuwahamasisha wawekezaji wengine kuwekeza katika fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa huo, ikiwa ni pamoja na sekta za madini, utalii, kilimo na usafirishaji.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika, naye aliipongeza Kampuni ya GBP kuwekeza katika wilaya hiyo – akisema ni sehemu sahihi kwa uwekezaji.

Mkuchika aliwahamasisha wananchi wa Butiama na mkoa wa Mara kwa ujumla kutumia kituo hicho cha mafuta katika kupata huduma mbalimbali za kisasa na mafuta yenye ubora wa uhakika.

Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji wa GBP Tanzania, Dawood Sadikot, alisema kampuni hiyo ina uzoefu wa uuzaji wa mafuta hapa nchini kwa miaka zaidi ya 25 na imeajiri watu zaidi ya 1,000.

“Ujenzi wa kituo hiki ni mwendelezo wa biashara zetu nchini Tanzania na tunaishukuru serikali kwa kuweka mazingira mazuri yanayowawezesha kuwekeza na kusaidia katika ujenzi wa Tanzania,” alisema Sadikot.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo inajivunia wafanyakazi wake wanaofanya kazi kwa nidhamu, uadilifu, weledi na kutoa huduma bora kwa wateja.

Hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Mafuta cha GBP Butiama ilehudhuliwa pia na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Butiama, Mbunge wa Jimbo la Butiama, Dkt. Charles Wilson Mahera, maafisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages