NEWS

Saturday, 1 August 2026

Tarime: Michango ya shilingi milioni 204 yakusanywa harambee ya ujenzi Kanisa la SDA Turwa



Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles (wa pili kushoto) na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete (kulia) na wageni wengine wakiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa la SDA Turwa jana.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Shilingi milioni 204 zimekusanywa katika harambee ya kuendeleza ujenzi wa jengo la Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Turwa lilipo katika mji wa Tarime, mkoani Mara.

Kiasi hicho cha fedha kinahusisha pia michango ya saruji mifuko 361 na mchanga tripu 12, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 12.5.

Harambee hiyo iliyofanyika Jumamosi, Agosti 1, 2026, ilihudhuriwa na washiriki wa kanisa hilo, viongozi wa serikali, dini na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara.

Wachangiaji wakubwa walikuwa familia ya Simion Kiles na marafiki zao waliotoa shilingi milioni 83, na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho ambaye alikuwa mgeni rasmi na kuwakilishwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete ambao kwa pamoja walitoa shilingi milioni 50.
Kiles na mke wake, Esther wakizunmza katika harambee hiyo

Hadi harambee hiyo inafanyika, tayari shilingi milioni 36 zilizochangwa na washiriki wa kanisa hilo zilikuwa zimewekwa benki, kwa mujibu wa Kiles.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Nyansaho, Chomete aliwashukuru watu wote waliojitokeza kufanikisha harambee ya mradi huo wa Kanisa la SDA Turwa kwa ajili ya kuimarisha huduma za kiroho.

Kwa upande wake Kiles ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mwaka 2020 - 2025, alisema: "Kwa kweli tunamshukuru Mungu harambee yetu imefanikiwa.”

Nao viongozi na washiriki wa Kanisa la SDA Turwa walishukuru wakisema fedha zilizopatikana zitatumika kuharakisha hatua zilizobaki za ujenzi wa jengo hilo ili lianze kutumika kwa shughuli za kiroho.

Walieleza kuwa nyumba za ibada kama hiyo inayojengwa zina nafasi kubwa katika kujenga maadili, amani na mshikamano wa jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages