NEWS

Sunday, 1 February 2026

Shinyanga: Waziri Mavunde azindua helikopta ya Barrick kwa ajili ya utafiti wa kisasa wa madini




Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya Barrick ambayo inaendesha shughuli zake kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Twiga Minerals imezindua helikopta itakayotumiwa kufanya utafiti wa wa kisasa wa kijiolojia wa anga wenye kupunguza athari za kimazingira na kuboresha shughuli za utafutaji wa madini nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, jana Jumapili Februari 1, 2026, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha sekta ya madini nchini na kufungua milango ya tafiti kwa kutumia nyenzo za kisasa zaidi.

Waziri Mavunde alisema uwekezaji wa teknolojia ya kisasa ni muhimu katika utekelezaji wa sera ya madini ya Taifa, inayolenga kuimarisha utafiti wa rasilimali madini, kuongeza thamani ya sekta ya madini katika uchumi wa taifa na kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa ufanisi zaidi.
“Ni moja ya hatua kubwa kwa Kampuni ya Barrick nchini kwa kushirikiana na Kampuni ya Twiga Minerals ya Serikali katika kufanya tafiti kwa njia ya kisayansi zaidi kwa lengo la kupanua wigo wa maeneo mapya ya utafiti na uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini,” alisisitiza.

Waziri Mavunde aliongeza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria katika kufanya tafiti kwa njia ya helikopta kwa sababu utafiti wa madini ni sayansi inayohitaji uwekezaji mkubwa.

"Kupitia Dira ya Madini 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kuhakikisha tunaongeza eneo la utafiti wa kina wa madini kupitia uwekezaji wa serikali na sekta binafsi"

"Tunachokifanya leo hapa ni kiashiria tosha kwamba maono hayo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanakwenda kufikiwa ipasavyo. Tunaishukuru Kampuni ya Barrick kwa kuamua kuunga mkono juhudi hizi za serikali kwa vitendo," alieleza Waziri Mavunde.

Alifafanua kuwa Barrick imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye tafiti na kwamba baada ya uzinduzi wa helikopta utafiti wake utagusa maeneo ya Nzega, Igunga, Msalala na Nyangh’wale katika mkoa wa Shinyanga.

“Naipongeza Barrick kwa kuendelea kuwekeza kwenye eneo la tafiti kwa sababu dunia ya leo huwezi kukwepa utafiti katika shughuli za madini,” alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, alisema ni hatua kubwa kwa kampuni hiyo kwa kushirikiana na serikali katika uzinduzi wa helikopta ya kisasa ya utafiti wa kijiolojia wa anga, itakayosaidia shughuli za utafutaji wa madini kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.

Dkt. Ngido aliongeza kuwa Barrick inatarajiwa kufanya utafiti wa kijiolojia wa kutumia teknolojia ya hali ya juu na kisasa zaidi (high-resolution airborne geophysical surveys) ambayo huongeza usahihi wa upatikanaji wa taarifa za miamba iliyo chini ya ardhi, kupunguza athari za kimazingira na kuboresha ufanisi wa shughuli hizo.

Alisema uzinduzi wa tafiti hiyo ambayo itatumia helikopta unaakisi dhamira ya Kampuni ya Barrick kuendelea kuwekeza nchini na kutafuta maeneo yatakayofaa kuanzisha migodi mikubwa ili kuleta mchango wa muda mrefu kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, alifafanua kuwa mchango wa Barrick katika utafutaji wa madini nchini, umeonekana kwa vitendo kupitia ushirikiano wake na serikali chini ya Wizara ya Madini na taasisi zake, na kwamba kampuni hiyo imekuwa mdau mkubwa katika shughuli za utafiti za kijiolojia, kutoa ushauri wa kitaalamu na kuwezeha upatikanaji wa taarifa za msingi za madini.

Kuhusu taarifa za tafiti zisizofaa kwa uchimbaji mkubwa, Dkt. Ngido alisema serikali imekuwa inazitumia kugawa maeneo kwa ajili wachimbaji wadogo na kuboresha ufanisi wao, sambamba na malengo ya serikali ya kurasimisha na kuendeleza sekta ya uchimbaji mdogo.

Mfano wa maeneo ambayo tafiti za Barrick zimetumiwa na wachimbaji wadogo ni Majimoto, Komarera na Golden Ridge ambapo shughuli za wachimbaji wadogo zimekuwa na tija.

“Kwa kipindi cha miaka mitano tayari tumewekeza Shilingi bilioni 100 katika kufanya utafiti wa kisayansi ili kuweza kugundua maeneo mapya kwa ajili ya uwekezaji mkubwa,” alisema Dkt. Ngido.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, alisisitiza kuwa serikali ya mkoa huo itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji waendelee kufanya kazi zao kwa ufanisi ili serikali iendelee kukusanya mapato.

Uzinduzi huo ni sehemu ya uwekezaji endelevu wa Barrick na Twiga katika kuboresha mbinu za utafiti na ugunduzi wa madini, kwa lengo la kupanua wigo wa rasilimali za madini na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages