NEWS

Monday, 2 February 2026

Musoma Vijijini wahitaji bilioni 120/- kutekeleza miradi mikubwa miwili ya kimkakati



Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, akizungumza Bungeni jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
---------------

Jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara linahitaji shilingi takriban bilioni 120 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa miwili ya kimkakati, Bunge limeambiwa.

Mbunge wa jimbo hilo, Prof. Sospeter Muhongo, aliyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita, akitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa barabara (km 40) sambamba na daraja la mto Suguti, na bwawa kubwa la umwagiliaji la Bugwema.

Prof. Muhongo alifafanua kuwa kwenye ujenzi wa barabara hiyo na daraja la mto Suguti wanahitaji shilingi bilioni 80, na kwenye bwawa la umwagiliaji la Bugwema zinahitajika shilingi takriban bilioni 42 ili miradi hiyo itekelezwe.

“Tulimwomba Mhe. Rais [Dkt. Samia Suluhu Hassan] akakubali… tunaendelea kufuatilia serikalini fedha zipatikane. Bwawa la Bugwema mkandarasi amepatikana, tunaomba tu serikali iendelee kutafuta fedha aanze kazi,” alisema.

Mbunge huyo wa Musoma Vijijini pia alimshukuru Rais Samia na serikali yake kwa kukubali ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 92 kwa kiwango cha lami katika jimbo hilo, na kwamba tayari imeshajengwa kilomita tano.

Kwa upande mwingine, Prof. Muhongo alisema katika miaka mitano ijayo serikali lazima iweke kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maji, umeme na barabara.

Akichangia hotuba ya Rais Samia aliyoitoa Bungeni Novemba 15, mwaka jana, Mbunge huyo alisema uenezaji wa huduma za maji, umeme na barabara ni muhimu katika kukuza ustawi wa wananchi.

Alisema hotuba ya Rais Samia imegusa maeneo muhimu ya uchumi, ajira na ustawi wa taifa ambayo yako kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025-2050.

Alieleza kuwa Rais Samia na serikali yake wamefanya mambo mengi makubwa "katika majimbo yetu" kwa kusukuma maendeleo ya kisekta vijijini.

Katika mchango wake, Prof. Muhongo alitilia mkazo uchangiaji wa mawazo ya utafutaji wa vyanzo vipya vya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya wananchi.

Jimbo la Musoma Vijijini lenye kata 21 na vijiji 68 ni moja ya maeneo yaliyopiga hatua ya maendeleo mkoani Mara, hususan katika sekta za kijamii kama vile afya, elimu, maji, umeme na barabara.

Nguvu za maendeleo katika jimbo hilo pia zimeelekezwa kwenye sekta za kilimo na uvuvi kandokando ya Ziwa Victoria.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages