Lori likiwa kazini katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara wilayani Tarime
Na Mwandishi Wetu
---------------------------
Katika kipindi cha miaka saba ya ushirikiano wa ubia wa Barrick-Twiga, yaani serikali na sekta binafsi, ni wazi kwamba mambo mengi yaliyofanyika kwenye tasnia ya madini yamechochea maendeleo ya taifa kiuchumi na kijamii.
Mafanikio makubwa yaliyotokana na ubia wa Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick, ni kielelezo tosha kwamba chini ya ushirikiano wa serikali na sekta binafsi, taifa lina uwezo mkubwa kuondoa vikwazo vinavyoathiri maendeleo yake kwa kila sekta ya shughuli binadamu.
Tumeshuhudia wazi jinsi ushirikiano wa Barrick-Twiga ulivyochangia ongezeko la ulipaji kodi serikalini, kuongezeka kwa gawio, mrabaha na kuchochea utekelezaji wa miradi ya kijamii katika sekta za elimu, afya, maji na barabara kupitia fedha za Uwajibikajii wa Kampuni kwa Jamii (CSR).
Vilevile, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa hadi mwaka jana asilimia 90 ya ununuzi wa bidhaa na huduma kwenye katika migodi ya Barrick nchini zinafanywa na kampuni za Watanzania wakiwemo wenyeji wa maeneo yanayopakana na migodi ya Barrick.
Aidha, asilimia 95 ya wafanyakazi katika migodi ya Barrick hapa nchini ni Watanzania ambao kati yao asilimia 49 wanatoka vijiji vilivyo jirani na migodi hiyo.
Licha ya ajira, wananchi waishio jirani na migodi wamenufaika kwa kuanzisha huduma na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo chimbuko lake kubwa ni kuwepo kwa migodi katika maeneo yao.
Kwa ujumla, ubia wa Barrick-Twiga tangu uundwe mwaka 2019 umeisaidia sana serikali kugharimia utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi kifupi cha karibu miaka saba iliyopita na kujenga ustawi kwa Tanzania mpya.
Katika kuonesha umakini wa ubia huo kwa maendeleo ya Tanzania tangu mwaka 2019, kampuni ya Barrick imewekeza dola za Marekani bilioni 4.79 katika uchumi wa taifa kupitia malipo ya kodi na tozo mbalimbali, gawio, mrabaha, mishahara na malipo ya wazabuni wa ndani.
Moja ya miradi ya mkakati inayotekelezwa kwa ubia wa Barrick-Twiga ni ule unaoitwa "Barrick-Twiga Future Forward Education Programme" wa kuboresha na kuongeza miundombinu ya shule za sekondari za serikali za kidato cha tano na cha sita kujenga mazingira bora ya kusomea.
Chini ya mradi huu, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vyumba vya madarasa, mabweni na mazingira mazuri ya kusomea ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Hill, ameeleza waziwazi kwamba kampuni yake itaendelea kutekeleza sera zake madhubuti zilizochochea mafaniko.
"Kanuni ambazo zimetuongoza kwa miaka mingi bado hazijabadilika; kuwaweka watu wetu salama, uchimbaji madini kwa uwajibikaji, kujenga ushirikiano imara na kutoa thamani ya muda mrefu ambayo inahusisha wadau wote," amesema Hill.
Somo kubwa tunalojifunza kama taifa kutokana na ushirikiano wa Barrrick-Twiga ni kwamba dhamira ya pamoja ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika nchi yoyote ile inayoongozwa kwa mwavuli imara wa sekta ya umma na sekta binafsi.
Ndiyo maana Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 imeweka bayana nafasi ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufikia pato la taifa la dola za Marekani trilioni moja (1,000,000,000,000).
Lengo la kufikia pato hilo 2050 ni kupunguza kama siyo kufuta kabisa umaskini katika jamii.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:
Post a Comment