
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya.
----------------------------
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya, ameendelea kujijengea heshima na kuaminika kwa wananchi kutokana na jitihada kubwa anazofanya katika kuleta na kusimamia maendeleo ya kisekta ndani ya jimbo hilo.
Miongoni mwa hatua za kwanza na za kihistoria alizochukua ni kuanzisha programu malum ya elimu kwa watoto wanaotoka familia zenye mazingira magumu, aliyoipa jina la Bulaya Community Education Program.
Kupitia programu hiyo, wanafunzi 331 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza walipata msaada wa kielimu, shilingi zaidi ya milioni 60 zilitumika kufanikisha ndoto za watoto hao.
Hatua hiyo imeleta faraja kubwa kwa wazazi na walezi, huku ikiweka msingi imara wa kuinua elimu ndani ya jimbo la Bunda Mjini.
Pia, Bulaya ameendelea kugusa maisha ya wananchi kwa kuchangia na kusimamia ukamilishaji wa majengo ya shule na zahanati katika kata mbalimbali, zikiwemo Nyasura, Balili, Bunda Stoo, Guta, Sazira, Wariku, Kabalimu, Mcharo na Kabasa.
Hatua hiyo imeongeza upatikanaji wa huduma za elimu na afya kwa wananchi, hususan wanawake, watoto na makundi yenye uhitaji maalum.
Mbunge huyo pia alipeleka vifaa vya kisasa vya kudurufu mitihani katika Shule ya Sekondari Nyamakokoto, hatua iliyoboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa biashara ndogondogo katika kuinua uchumi wa wananchi, Bulaya aliwezesha uwekaji wa taa za kisasa katika Soko la Genge la Jioni, jambo lililoongeza usalama na muda wa kufanya biashara kwa wafanyabiashara.
Mbali na juhudi zake jimboni, Mbunge Bulaya ameendelea kuwa sauti ya wananchi wa Bunda Mjini ndani ya Bunge la 13, Mkutano wa Pili, ambapo aliweza kuuliza maswali na kuibua hoja zinazolenga maendeleo ya jimbo hilo.
Miongoni mwa masuala aliyoyasimamia ni pamoja na hatma na utekelezaji wa mradi wa TACT, uboreshaji wa Soko la Manjebe, ujenzi wa chumba cha OPD na wodi ya wanaume na changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya pembezoni mwa mji wa Bunda.
Kwa upande mwingine, aliishauri serikali kusaidia wawekezaji katika eneo tengefu la EPZ lililopo mtaa wa Tairo katani Guta, pamoja na suala la wakazi wa Nyatwali.
Kwa ujumla, Mbunge Bulaya ameendelea kuthibitisha kuwa ni kiongozi mwenye maono, anayesimamia kwa vitendo kaulimbiu ya maendeleo jumuishi, huku akitanguliza maslahi ya wananchi wa Bunda Mjini.
Wana-Bunda wana kila sababu ya kujivunia uongozi wa Mbunge Esther Bulaya kwa uwajibikaji, ushirikishaji na mapambano ya kweli kwa maendeleo ya jamii nzima.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment