NEWS

Sunday, 8 February 2026

Rais Samia: Tutajenga Reli ya Tanga–Musoma kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za kibiashara



Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Ikulu jijini Dar es Salaam, jana Jumamosi.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
---------------------

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itajenga reli kutoka mkoa wa Tanga hadi Musoma mkoani Mara, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma za kibiashara.

Amesema reli hiyo itaiwezesha Tanzania kutumia kikamilifu nafasi yake ya kijiografia kwa kuunganisha Bandari ya Tanga na Ziwa Victoria, hivyo kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda Uganda na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

“Tanzania kipindi hiki cha 2025-2030 tuna nia ya kujenga reli itakayounganisha Tanga hadi Musoma, na kule [Musoma] watasafirisha kwa ziwa [Victoria] kwenda Uganda,” alisema.

Rais Samia alisema hayo jana Jumamosi Ikulu jijini Dar es Salaam, katika mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambapo viongozi hao pia walisisitiza dhamira ya nchi zao kuendeleza ushirikiano wa karibu katika miradi ya kimkakati ya kiuchumi na kiusalama.

Katika mazungumzo hayo, Tanzania na Uganda zilikubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano katika miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), ambao ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kihistoria barani Afrika.

Mradi huo ambao unaokaribia kukamilika, unatajwa kuwa nguzo muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, na kuchochea ajira, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa kikanda.

Rais Samia alisema serikali za Tanzania na Uganda zimeendelea kuondoa vikwazo vya kibiashara na kuweka mazingira rafiki kwa lengo la kujenga soko imara la Afrika Mashariki, sambamba na kuendeleza miradi ya pamoja ya uzalishaji nishati kwa manufaa ya nchi hizo.

“Tumekuwa tukiviondosha vikwazo vya kibiashara na kutengeneza soko la Afrika Mashariki, kuendelea kuzalisha nishati kwenye miradi ya ushirikiano kwa ajili ya matumizi yetu ndani ya nchi zetu hizi mbili,” alisema Rais Samia.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages