NEWS

Sunday, 1 February 2026

Naibu Waziri wa Madini awahakikishia wachimbaji wadogo Tarime kuwa watanufaika na programu ya MBT



Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, akizungumza na wachimbaji wadogo katika kikao kilichofanyika Nyamongo, wilayani Tarime jana Jumamosi. aaliyekaa kushoto mbele ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Meja Edward Gowele.

Na Godfrey Marwa,
Tarime
-------------

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, jana Jumamosi Januari 31, 2026 alifanya ziara ya siku moja katika wilaya ya Tarime, mkoani Mara na kufanya mazungumzo na wachimbaji wadogo katika eneo Nyamongo.

Dkt. Kiruswa aliwahakikishia wachambaji hao kuwa watanufaika na programu ya Mining For A Brighter Tomorrow (MBT) awamu ya pili.

Kwa mujibu wa Dkt. Kiruswa, serikali itatenga bajeti ya kutekeleza mradi huo mara baada ya andiko lake kuwasilishwa wiozarani.

“Nimekuja kuonesha nia ya dhati ya serikali, mradi huu haujasahaulika wala kuchelewa - upo katika hatua zake sahihi, kinachohitajika ni uvumilivu, mradi haujatoka kwenye mstari, uko relini," Naibu Waziri Kiruswa aliwahakikishia wachambaji hao.


Sehemu ya wachimbaji hao wakiwa katika kikao na Naibu Waziri Kiruswa

Kikao hicho kililenga kusikiliza changamoto kwa ajili ya kuzitatua ili kuharakisha kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kunufaisha mamia ya vijana kutoka vijiji 13 vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

“Sisi kama wizara tunatamani hii kazi iende kwa kasi na ndio maana nimekuja hapa leo,” alisisitiza Naibu Waziri Kiruswa.

Tayari vikundi vya wachimbaji hao vimeshapewa mafunzo maalumu kwa ajili ya kuanza shughuli za uchambaji wa madini, kwa mujibu wa Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Hamad Kallaye.

“Changamoto kuu ni ukosefu wa fedha za kuendesha mradi na baadhi ya leseni kubainika kuwa katika makazi ya watu," Mhandisi Kallaye alisema katika sehemu ya taarifa yake kwa Naibu Waziri Kiruswa.


Mhandisi Kallaye akizungumza katika kikao hicho

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Kiruswa alifuatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, miongoni mwa wengine.

Programu ya MBT inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kiuchumi, hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum, ambapo uzinduzi wake rasmi unatarajiwa kufanyika Februari 2026.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages