NEWS

Friday, 31 July 2026

RC Mara apokea magari matatu mapya kutoka serikalini



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kuanza kutumika kwa magari mapya aliyopokea leo kutoka serikalini.

Na Godfrey Marwa
Musoma
-------------

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara imepokea magari matatu mapya yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya kurahisisha utendaji shughuli za kuhudumia wananchi, yaliyonunuliwa na serikali kwa nyakati tofauti kupitia Wakala wa Ununuzi na Ugavi Serikalini (PGSA).

Akizungumza wakati wa mapokezi ya magari hayo mjini Musoma leo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amemshukuru Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitaja hatua hiyo kama ushahidi wa nia yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi.

"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia, huu ni Ushahidi kuwa amejipanga kuhakikisha kuwa serikali inawatumikia wananchi,” amesema.

Baada ya kupokea magari hayo, Kanali Mtambi ameyakabidhi kwa Katibu Tawala wa mkoa huo, Gerald Kusaya, na kusisitiza umuhimu wa kuyatunza vizuri na kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kanali Mtambi (kushoto) akimkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa, Gerald Kusaya, funguo za magari hayo.


Magari mapya yaliyopokewa leo

"Tunapopata vitendea kazi inakuwa faraja kwetu, vinatuwezesha kutekeleza na kutimiza wajibu. Tuvitumie vitendea kazi hivi vizuri kwa maana ya kuwahi kwenye maeneo tunapokwenda kuwatumikia wananchi.

"Tulikuwa tukiomba magari ila sasa tunayo, yasipotunzwa na kutumika kwa matumizi sahihi itakuwa ni hujuma. Tuhakikishe tunayatunza ili kufikia malengo ya serikali ya kuwatumikia wananchi,” amesisitiza Kanali Mtambi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages