
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akiagiza kiagiza wasimamizi wa ujenzi ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wakamatwe na kuhojiwa.
Muheza
---------------
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza wajumbe wa kamati za mapokezi na ujenzi za mradi wa ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wakamatwe na kuhojiwa mara moja ili watoe taarifa juu ya upotevu wa vifaa vya mradi huo.
Dkt. Mwigulu alitoa agizo hilo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Lusanga, kata ya Mgomeni, wilayani Muheza waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ofisi hiyo itakayokuwa na ghorofa moja pindi ikikamilika.

“Kuna nondo 700, marine boards 500 na matofali 2,000... hivi vifaa havijulikani viko wapi. Wahusika kila siku mnaripoti kazini, na mishahara mnalipwa wakati ujenzi umesimama na hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Jumaa Mhina.
Aliendelea: “Kamanda wa TAKUKURU ninahitaji hii taarifa kwa kina kabla sijamaliza ziara yangu mkoani Tanga. OCD (Mkuu wa Polisi wa Kituo) fuatilieni kwa kina ushiriki wa watumishi wa hii halmashauri. Kila mmoja ahojiwe hadi tujue vifaa vilipoteaje.”
Waziri Mkuu Mwigulu alisema anazo taarifa kwamba timu ya manunuzi imenunua vifaa ambavyo vimewekwa stoo wakati hatua yake ya ujenzi haijafikiwa.
“Nimeambiwa vifaa vingine vimekuja lakini vimekaa stoo. Ni kwanini mmenunua wakati hamjamaliza hatua ya kwanza? Mshauri mwelekezi wa mradi yupo lakini hamsikilizi ushauri anaotoa,” alihoji.

Jengo hilo ndiyo limemalizika kujengwa ghorofa ya chini, na linasubiri kuanza kuwekewa linta kwenye ghorofa ya kwanza.
Waziri Mkuu alikemea tabia ya kutochukua hatua katika masuala kama hayo yanapojitokeza, hasa ikizingatiwa kwamba halmashauri nyingine ambazo walipewa fedha kwa wakati mmoja wao wameshakamilisha ujenzi.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu na Maendeleo Mijini na Vijijini, Mhandisi Abdalla Jaha, alisema mradi huo ambao umefikia asilimia 68, ulianza kujengwa Septemba 29, 2023 na wanatarajia ifikapo mwishoni mwa Juni, 2026 sakafu ya chini ianze kutumika.
No comments:
Post a Comment