NEWS

Friday, 20 March 2026

RC Mtambi aipongeza TAKUKURU Mara kwa ushirikiano inaotoa usimamizi wa miradi



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (kulia), akiwa katika mahojiano ya vipindi vya televisheni vinavyoratibiwa na TAKUKURU jijini Dodoma, jana.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
------------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, ameipongeza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara kwa ushirikiano inaotoa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

RC Mtambi alitoa pongezi hizo jana Alhamisi jijini Dodoma wakati wa mahojiano ya vipindi vya televisheni vinavyoratibiwa na TAKUKURU.

“TAKUKURU inatusaidia sana kufanya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, ni jicho letu katika kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na katika ubora unaotakiwa,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na kazi inayofanywa na TAKUKURU, wananchi wa mkoani Mara wana uhakika wa miradi yao kutekelezwa vizuri, kupata huduma bora na kupunguza mianya ya rushwa.

Alitoa mfano Shule ya Sekondari Kasoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, ambayo awali ilikuwa inatumia kuni kupika chakula lakini baada ya ufuatiliaji wa TAKUKURU na kuwashirikisha wadau wa maendeleo kwa sasa inatumia nishati safi ya kupikia.

Mkuu huyo wa mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuwapongeza wananchi wa mkoa wa Mara wanaoshiriki katika usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Alisema wananchi wamesaidia sana katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuchangia fedha, nguvu kazi, kufanya ufuatiliaji na kutoa taarifa pale wanapoona kuna tatizo kwenye utekelezaji.


RC Mtambi (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Afisa wa TAKUKURU jijini Dodoma, jana.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages