NEWS

Tuesday, 24 March 2026

Sekta ya madini yachangia asilimia 12.7 Pato la Taifa




Na Mwandishi Wetu
Dodoma
---------------

Sekta ya madini nchini imeendelea kuonesha mwelekeo chanya wa ukuaji wa uchumi, baada ya kuchangia asilimia 12.7 ya Pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2025.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, wakati akifungua Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2025/2026, lililofanyika jijini Dodoma, leo Machi 24, 2026.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amesema thamani ya mauzo ya mazao ya madini nje ya nchi kwa mwaka 2025 imefikia dola za Kimarekani milioni 4,119 sawa na shilingi zaidi ya trilioni 10.3 za Kitanzania.

Katibu Mkuu Samamba amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya madini, hususan kupitia uanzishaji na uboreshaji wa masoko ya madini pamoja na mikakati madhubuti ya kudhibiti utoroshaji wa madini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwakilishi wa Afisa Kazi Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmary, amesema Ofisi ya Kamishna wa Kazi inajivunia ushirikiano na mafanikio ya Wizara ya Madini katika kuzingatia masuala ya haki na ustawi wa wafanyakazi.

Naye Mwakilishi wa TUGHE Taifa, Happiness Kitarima, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazotekeleza kwa vitendo misingi na kanuni za chama hicho, ikiwemo kulinda maslahi ya watumishi na kuimarisha mahusiano kazini.

Kwa ujumla, sekta ya madini inaendelea kuwa miongoni mwa mihimili muhimu katika ajenda ya maendeleo ya uchumi wa viwanda na uwekezaji Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages