=

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo (aliyevaa suruali ya kaki), akimshukuru Mwenyekiti wa Nyansaho Foundation na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, aliyekabidhi saruji mifuko 6,000 kwa wabunge 12 wa mkoa wa Mara, mjini Musoma jana. Nyuma yao ni lori lililobeba shehena ya saruji hiyo.
Musoma
------------------
Katika kuchochea maendeleo ya jamii kwa vitendo, Taasisi ya Nyansaho (Nyansaho Foundatio) imegawa saruji mifuko 6,000 kwa wabunge 12 wa mkoa wa Mara, wakiwemo wa viti maalum.
Mwenyekiti wa Nyansaho Foundation, Dkt. Rhimo Nyansaho ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alikabidhi saruji hiyo katika hafla iliyofanyika mjini Musoma, jana.
“Tutatoa mifuko ya cement (saruji) elfu sita na mgawanyo utaenda siyo kwa kila jimbo, ni kwa kila mbunge. Kwa hiyo, wabunge 12 nikitoka mimi, kila mmoja atapata mifuko 500,” Dkt. Nyansaho alisema wakati wa makabidhiano hayo.
Alielekeza saruji hiyo ielekezwe kwenye ujenzi na ukarabati wa miradi ya elimu na afya katika majimbo yote ya mkoa wa Mara ili kuboresha huduma kwa wananchi.
“Kila mbunge aseme hii mifuko itaenda kufanya moja, mbili, tatu. Tukishafanya vile, kamati ya usalama kupitia kwa wakuu wa wilaya na RC (Mkuu wa Mkoa) akiwa ndiye coordinator (mratibu) inatolewa taarifa,” alielekeza.
Aidha, Dkt. Nyansaho aliahidi kurudi kugawa mabati kwa wabunge hao kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo, hususan kwa wale watakaokuwa wamefanikiwa kujenga maboma ya majengo yanayohitajika.
“Baada ya siku 60 kuanzia sasa tupate taarifa kwamba ile mifuko 6,000 imefanya maboma… Tukimaliza Bunge la Bajeti nitakuwa nimeshajipanga kupitia kwa wadau - tutawaletea mabati, sasa ili uletewe mabati mpaka tuone boma,” alisema.
Kwa upande wao, wabunge hao walimshukuru Mwenyekiti huyo wa Nyansaho Foundation wakisema hatua hiyo itachochea kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi wa mkoa wa Mara.
Sambamba na hilo, wabunge hao waliahidi kusimamia kikamilifu matumizi sahihi ya saruji hiyo ili kuhakikisha inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.
“Kwa hii nguvu ambayo umetuongezea tukuhakikishie hatutakuvunja moyo,” alisema Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel.
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya, naye alimshukuru Dkt. Nyansaho na kumuahidi ushirikiano wa dhati sambamba na kumwombea baraka za Mungu.
“Nyansaho umekuwa ukijitoa sana kwa ajili ya mkoa wako, sisi wabunge wenzako tutakupa ushirikiano, tutakuombea kwa Mwenyezi Mungu, tunajua Nyansaho Foundation inafanya kazi kubwa sana si katika mkoa wetu lakini pia maeneo mbalimbali nchi nzima,” alisema Bulaya.
Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, alimshukuru Dkt. Nyansaho akisema: “Kwa huu mchango ambao umeleta, umemfanya kila mbunge ataenda jimboni akiwa na jambo.”

Wabunge wa mkoani Mara wakiwa na sehemu ya saruji mifuko 6,000 ambayo iliotolewa na Nyansaho Foundation, katika picha ya pamoja na Dkt. Rhimo Nyansaho (aliyevaa shati jeuzi).
Hafla hiyo ya makabidhiano ya saruji ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, miongoni mwa wengine.
Mkoa wa Mara unaundwa na majimbo 10 ya uchaguzi; ambayo ni Musoma Mjini, Musoma Vijijini, Butiama, Rorya, Tarime Mjini, Tarime Vijijini, Serengeti, Bunda Mjini, Bunda Vijijini na Mwibara.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment