
Na Mwandishi Wetu
---------------------------
---------------------------
Tanzania inazidi kung'ara kwa kushika nafasi ya nne barani Afrika katika kuwavutia wawekezaji sekta ya madini.
Katika uwekezaji kwenye sekta hiyo, Tanzania inatanguliwa na nchi za Botswana, Morocco na Zambia.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Fraser Institute, Annual Survey of Mining Companies 2025, Tanzania inashika nafasi ya 34 kati ya maeneo 68 duniani yaliyotathminiwa Investment Attractiveness Index (IAI), kielelezo kinachotumiwa na wawekezaji na kampuni za utafiti wa madini kuamua wapi waelekeze mitaji ya utafiti na maendeleo ya miradi.
Ripoti hiyo inaonesha kumekuwepo na mwenendo chanya wa kupanda kwa alama za Tanzania, ambapo imefikia 68.04 mwaka 2025, ikilinganishwa na 62.75 mwaka 2024 na 46.38 mwaka 2023.
Wataalamu wa madini wanaeleza IAI hujengwa kwa kuzingatia vipengele vikuu viwili vinavyoongoza maamuzi ya uwekezaji.
Vipengele hivyo ni uwezo wa kijiolojia wa rasilimali na mazingira ya jumla ya kufanya biashara kwenye sekta husika.
Ripoti inaeleza kuwa asilimia 60 ya uzito huenda kwenye uwezo wa kijiolojia wa rasilimali na asilimia 40 huenda kwenye sera ili kutoa taswira ya mvuto wa eneo husika kwa uwekezaji wa utafiti na uchimbaji.
Katika kipengele kinachoangalia mvuto wa jiolojia iwapo eneo lingekuwa na kanuni bora zaidi duniani, Tanzania imeorodheshwa nafasi ya 15 duniani kwa alama 75.00.
Takwimu hizo zinaonesha kwa uwazi ukubwa wa fursa na uwezo wa rasilimali nchini.
Utafiti huu wa Fraser Institute hutumiwa kimataifa na sekta binafsi, taasisi za utafiti na wadau kutathmini mwenendo wa masoko ya uwekezaji wa madini.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment